Sunday, October 2, 2016

DC TUNDURU AWATAKA VIONGOZI WA KIJIJI KUREJESHA FEDHA ZA WANANCHI

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lijombo wilayani humo.

Na Muhidin Amri,       
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru Juma Homera, ametoa siku saba kwa viongozi wa kijiji cha Lijombo wilayani humo kuhakikisha kwamba wanarejesha fedha kiasi cha shilingi 999,500 ambazo waligawana, huku wakijua kwamba fedha hizo ni za serikali ambazo zililenga kutekeleza miradi  ya maendeleo kijijini humo.

Homera alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho, ambao ulilenga kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi na viongozi wao wa kijiji juu ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Kijiji cha Lijombo kimeingia katika mgogoro huo kufuatia wananchi hao kuwatuhumu viongozi wao, kwa matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo kutafuna fedha pamoja na kushindwa kutoa taarifa za mapato na matumizi na kusababisha wananchi kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo.


Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru amewataka viongozi hao kurudisha haraka fedha hizo kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria, kwani wamesababisha kusimama kwa baadhi ya miradi kutokana na vitendo hivyo vya ubadhirifu wa fedha za wananchi.

Pia Homera ameagiza kwamba kuna fedha shilingi 300,00 ambazo walipewa kwa ajili ya kuwasaidia wazee nazo zirejeshwe haraka, kupitia akaunti ya kijiji hicho ili walengwa waweze kupewa na ziwasaidie katika kujikwamua kwenye maisha yao.

Awali wakitoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu huyo wa wilaya wananchi hao walisema kwamba mambo hayo yanayofanywa na viongozi wao ndiyo chanzo kikubwa cha kuathiri maendeleo ya wananchi, yasiweze kusonga mbele kutokana na kukosa uaminifu hasa katika matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali.

Walibainisha kuwa wamekuwa na mazoea viongozi wao kujifungia ofisini peke yao na kutoa maamuzi bila kushirikisha wananchi, ndiyo maana wanalalamikiwa na wananchi kufikia hatua hata ya kususia kufanya shughuli za kimaendeleo.

No comments: