Saturday, October 29, 2016

MANISPAA SONGEA YALALAMIKIWA KWA KUSHINDWA KUTENGA MAENEO YA MAEGESHO VYOMBO VYA USAFIRI

Ofisi za Halmashauri Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.


Na Muhidin Amri,              
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imelalamikiwa kwa kushindwa kwake kutenga maeneo rasmi ya maegesho ya magari hususani Malori na pikipiki, kitendo ambacho hivi sasa kinasababisha msongamano mkubwa wa vyombo hivyo vya moto kwa watu wanaotembea kwa miguu.

Pikipiki maarufu kama Yeboyebo, bajaji na magari ya mizigo yamekuwa yakipaki hovyo bila kufuata utaratibu maalumu katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo kama vile eneo maarufu la Ikweta, ambalo kuna makazi ya watu na nyumba za ibada.

Wakizungumza na gazeti hili  jana, baadhi ya wakazi hao walisema kuwa hali hiyo inawasababishia usumbufu mkubwa wakati wanapohitaji huduma ya usafiri kwani hakuna maeneo rafiki ambayo Manispaa hiyo imetenga kwa ajili ya kupata huduma ya usafiri kama vile boda boda, bajaji na malori.


Walisema kuwa kutokana na madereva hao kuachwa kiholela, kunawafanya wakati mwingine kuwa na hofu kutokana na hasa kwa madereva wa pikipiki kujihusisha na vitendo vya wizi, kwani wengi wao hawana sare na wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwa kutembea barabarani.

Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Songea, Ally Ngonyani alieleza kuwa tangu Manispaa hiyo iwahamishe madereva wa bajaji eneo la Soko kuu na wale wa malori kutoka katika eneo la mtaa wa Majengo mitumbani kumekuwa na usumbufu mkubwa, hatua ambayo inawafanya abiria washindwe kutumia usafiri huo ambao awali ulikuwa ni rahisi zaidi kwao.

“Pia tuna hofu kubwa ya kugongwa na boda boda, kwa sababu boda boda nyingi hazitulii katika eneo maalumu badala yake hutembea hovyo mitaani kwa ajili ya kutafuta wateja, jambo ambalo limekuwa likisababisha ajali nyingi na za mara kwa mara”, alisema Ngonyani.

No comments: