Wednesday, October 26, 2016

MANISPAA SONGEA YAPOKEA FEDHA ZA UTEKELEZAJI PROGRAMU YA UBORESHAJI MIJI NA MANISPAA

Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,            
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepokea zaidi ya shilingi bilioni 7.54 kwa ajili ya kutekeleza programu ya uboreshaji wa Miji na Manispaa (ULGSP).

Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha hizo ambazo zimepokelewa na Manispaa hiyo zimetoka hazina kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kwamba zimeletwa kwa awamu mbili.

Midelo alisema kuwa fedha zilizoletwa kwa awamu ya kwanza zilipokelewa mwezi Mei mwaka huu, kiasi cha shilingi bilioni 2.72 na awamu ya pili zilipokelewa Oktoba 6 mwaka huu kiasi cha shilingi bilioni 4.82.


Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Manispaa ya Songea kupitia programu ya ULGSP ilipanga kutekeleza miradi yake minne ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilometa 4.7 na fedha zingine zitatumika kwa ajili ya kuijengea uwezo halmashauri hiyo.

Manispaa ya Songea ni miongoni mwa halmashauri 18 hapa nchini, ambazo zinatekeleza mradi wa uboreshaji wa Miji na Manispaa ambapo mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018.

“Katika kipindi cha miaka mitano halmashauri yetu Manispaa ya Songea imepanga kutekeleza miradi nane yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 21’’, alisema Midelo.

Amelitaja lengo la mradi huo kuwa ni kuziwezesha halmashauri zilizomo kwenye mradi, kuboresha utendaji kazi kwa lengo la kutoa huduma bora na endelevu kwa jamii inayohudumiwa.


Hata hivyo alisema kuwa mradi umedhamiria kuongeza mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa mapato, kuimarisha uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo ya serikali, ujenzi wa miundombinu, kuongeza uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali za halmashauri na kujenga uwezo ndani ya halmashauri hiyo.

No comments: