Wednesday, May 24, 2017

AKUTWA AMEFARIKI DUNIA KWENYE NYUMBA YA KULALA WAGENI

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

ASHA Rais (41) ambaye ni mkazi wa Newala mkoani Mtwara, amekutwa akiwa amefariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni ambayo ipo karibu na uwanja wa michezo wa Majimaji, katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya jioni kwenye nyumba ya kulala wageni inayofahamika kwa jina la Salama, ambayo ipo kwenye kata ya Mfaranyaki mjini hapa.

Mwombeji alisema kuwa inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio hilo kutokea, Asha alikuwa amepanga chumba namba 412 katika nyumba hiyo ya kulala wageni ambako baadaye aligundulika akiwa amefariki dunia katika chumba hicho.


Alifafanua kuwa Asha alikuwa safarini akitokea Newala akielekea Mbeya na kwamba alipofika Songea alilazimika kulala ili siku inayofuata aendelee na safari yake, ambapo wahudumu wa nyumba hiyo walishtuka kuona toka mgeni wao aingie ndani hatoki.

Pia aliongeza kuwa kimya hicho kilipowashtua ndipo walipoamua kugonga mlango ili afungue lakini haukufunguliwa, ndipo walipoamua kwenda Polisi kutoa taarifa na askari walipowasili katika eneo la tukio na kuuvunja waliukuta mwili wa Asha ukiwa umelala kitandani na hauna jeraha lolote.


Hata hivyo taratibu zilipofanywa kwa kushirikiana na mganga aliyetoka hospital ya mkoa wa Ruvuma na kuufanyia uchunguzi mwili huo, ndipo ilibainika kwamba amefariki dunia na kwamba uchunguzi wa kifo chake unaendelea kuchunguzwa na jeshi la Polisi la mkoa huo ili kuweza kujua zaidi undani wa kifo chake.

No comments: