Wednesday, May 10, 2017

JANUARI HADI DISEMBA MALARIA MANISPAA SONGEA YAUA WATU 87

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

IMEBAINISHWA kuwa ugonjwa hatari wa malaria katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana, katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umesababisha vifo vya watu 87 sawa na asilimia 10.9 ya vifo vyote 798 vilivyotokea kutokana na magonjwa mengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyomfikia mwandishi wetu kutoka kwa Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa katika vifo hivyo watoto chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na ugonjwa wa malaria walikuwa 34 ambao ni sawa na asilimia tisa ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambavyo vilikuwa 401.

Midelo alisema kuwa mwaka 2016 Manispaa ya Songea ilikuwa na wagonjwa wa malaria waliopata matibabu ya nje 5,928 ambao ni sawa na asilimia 2.4 ya wagonjwa wote 244,245 waliopata matibabu ya nje.

Alisema kuwa wagonjwa waliogua ugonjwa wa malaria na kulazwa kwa mwaka huo ni sawa na asilimia 2.5 ya wagonjwa wote  244,425 waliolazwa.


Pia aliongeza kuwa watoto chini ya umri wa miaka mitano waliougua ugonjwa wa malaria na kutibiwa kwa matibabu ya nje walikuwa 2,258 sawa na asilimia 3.3 ya wagonjwa wote 68,796 chini ya miaka mitano na wale waliolazwa  ni watoto 2,374 sawa na asilimia 3.1 ya watoto wote waliougua ugonjwa huo.

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, Manispaa imejiwekea mikakati ambapo baadhi yake ni kuendelea kushirikiana na serikali katika kuendesha zoezi la mpango wa ugawaji wa vyandarua shuleni, akina mama wajawazito wakiwemo na watoto wadogo.

Mikakati mingine ameitaja kuwa ni kuendelea kununua dawa, vipimo vya kutosha vya (MRDT) na kusambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, utoaji elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua, kupima kabla ya kutibiwa, kuwahi matibabu mara unapoona dalili za malaria, kuwahi kliniki na kuweka mazingira ya kuishi katika hali ya usafi.

Afisa habari huyo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea itaendelea pia kushirikisha wadau mbalimbali katika kudhibiti ugonjwa wa malaria, kutoa tiba tahadhari kwa akina mama wajazito, kufanya ufuatiliaji, usimamizi na tathmini ya mwenendo wa ugonjwa wa malaria na kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria wakazi wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za afya na usafi wa mazingira.


Katika hatua nyingine jitihada ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria, Manispaa ya Songea imeanzisha mradi wa kugawa vyandarua bure kwa wazee 1,000 wasiokuwa na uwezo wa kununua vyandarua kutoka katika kata zote 21 zilizopo mjini hapa.

No comments: