Monday, May 29, 2017

WAUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS DKT. JOHN MAGUFULI

Na Dustan Ndunguru,
Geita.

WACHIMBAJI wadogo wa madini katika migodi ya Kakola na Nyakagwe wilaya ya Kahama na Geita mkoani Geita, wamesema kuwa uamuzi aliochukua Rais Dkt. John Magufuli wa kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza Makontena yenye mchanga wenye madini ulikuwa ni wa busara kutokana na ukweli kwamba mchanga huo uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, ulikuwa wenye madini jambo ambalo lilikuwa likisababisha nchi kukosa mapato yake.

Dkt. John Magufuli.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wachimbaji wadogo, Robert Nyamaigolo na Golod Makinga walisema kuwa kila Mtanzania ambaye ana uzalendo wa kweli anapaswa kupongeza jitihada hizo zilizofanywa na Dkt. Magufuli baada ya kumaliza kazi hiyo na kuchukua hatua.

Nyamaigolo alisema uzoefu unaonesha kuwa miaka mingi tume za kuchunguza masuala mbalimbali zilizokuwa zikiundwa zilikuwa hazitoi majibu yenye kuzaa matunda na baadaye wananchi walikuwa wakikosa imani na serikali yao.

“Rais Magufuli ameunda tume ya kuchunguza tatizo hili, mara ilipobainika kulikuwa na uzembe kwa watendaji husika ambao wameufanya mara moja amechukua hatua ya kuwawajibisha, ni jambo ambalo anapaswa kupongezwa hasa kwa Watanzania ambao ni wazalendo na wenye uchungu na rasilimali za nchi yao”, alisema Nyamaigolo.


Nyamaigolo alifafanua kuwa ni miaka mingi imepita Makontena yenye mchanga wa madini yalikuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi, ambapo wao kama wachimbaji wadogo hawakuwa na sauti ya kulizungumzia hilo kutokana na ukweli kwamba wawekezaji kwenye migodi hiyo walikuwa wamepewa kibali cha kusafirisha mchanga huo wenye madini.

“Sisi kama wachimbaji wadogo tuna ushahidi wa kutosha kuhusiana na mchanga huu uliokuwa ukisafirishwa kwa muda mrefu kabla hata Rais Dkt. Magufuli hajasitisha kusafirishwa huku, kilichotupatia uhakika ni kwamba madini yalikuwa yanaondoka huku tukiyaona kwa macho yetu na vilevile ni kile kitendo cha Kontena moja lenye mchanga kudondoka na mchanga wenye madini katika eneo la Segese huko Kahama”, alisema Nyamaigolo.

Alibainisha kuwa mara baada ya Kontena hilo kudondoka, wachimbaji wadogo walikuwa wakiuziwa mchanga ambapo walikuwa wakiendelea na kazi ya uchakataji ambapo kilichotokea katika mchanga huo, waliweza kupata dhahabu ya kutosha na ndipo walipokuwa na uhakika wa kile ambacho kinasafirishwa ni madini ya dhahabu na sio vinginevyo.

Mchimbaji huyo alieleza kuwa hata kabla ya Kontena hilo kudondoka madereva waliokuwa wakiendesha Makontena yenye mchanga wa madini walikuwa wakiwauzia mchanga huo wachimbaji wadogo kulingana na kiasi cha fedha walichonacho na kuweza kujipatia dhahabu.

Nyamaigolo alisema kuwa kutokana na hilo ni vyema serikali ikawashirikisha wachimbaji wadogo pale ambapo panahitajika kufanya uchunguzi kuhusiana na jambo lolote lile linalohusu madini, hususan katika sakata la sasa la usafirishaji wa mchanga wenye madini na kwamba Watanzania wanapaswa pia kufahamu wazi kuwa ni kweli nchi ilikuwa ikiibiwa madini mengi.

Naye Golod Makinga aliwaasa Watanzania kuunga mkono jitihada hizo zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika kupambana na wale wote ambao kwa miaka mingi walikuwa wakinufaika na rasilimali zilizopo hapa nchini kwa njia ya isiyo halali na kuwaacha wengi wakiwa maskini na kwamba aliiomba serikali kutoruhusu tena mchanga wenye madini kusafirishwa kwenda nje ya nchi badala yake kila jambo lifanyike ndani ya nchi kwa lengo la kuongeza mapato na ajira.


Makinga aliongeza kuwa serikali inaowajibu wa kuhakikisha kwamba inaendelea kuwalinda wachimbaji wadogo kutokana na ukweli kwamba hiyo ndiyo ajira yao ambayo imekuwa ikiwafanya waweze kuendesha maisha yao ya kila siku na isisite kuwaunga mkono kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ambavyo vitawasaidia katika shughuli zao za uchimbaji wa kila siku.

No comments: