Friday, May 19, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI WAMUOMBA KUINGILIA KATI UJENZI MRADI WA MAJI MKAKO MBINGA

Rais Dokta John Magufuli.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MRADI wa maji ambao umejengwa katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, umeendelea kuingia dosari na kuchukua sura mpya baada ya Wananchi wa kata hiyo kuendelea kulalamikia kwamba mradi huo umekuwa ukitoa maji machafu ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Kadhalika licha ya kuunyoshea kidole kwamba unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika, bado wakazi hao wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuingilia kati na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohusika na usimamizi mbovu juu ya mchakato wa ujenzi wa mradi huo.

Baadhi yao wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa kuomba majina yao yasitajwe katika mtandao huu walisema kuwa wameshangazwa na serikali kwa kutochukua hatua za haraka licha ya kulalamikia jambo hilo kwa muda mrefu, hadi ilipofikia hatua ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour kutoa agizo lake Mei 8 mwaka huu kwa kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aunde Kamati ya kushughulikia suala hilo na kumpatia majibu haraka iwezekanavyo.


Walisema kuwa mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike mapema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa, lakini inashangaza kuona kwamba hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na sehemu kubwa ya fedha za mradi huo zimekwisha tumika.

“Mradi huu tumekuwa tukiulalamikia siku nyingi miaka mingi iliyopita lakini hakuna hatua zilizokuwa zikichukuliwa, leo mpaka anakuja kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kutoa amri ya kushughulikia suala hili ndiyo linashughulikiwa, kwa kweli inatuuma sana”, walisema.

Walidai kuwa wanaimani kwamba matumizi ya fedha hizo katika mradi huo wa maji zilikuwa zikitumika vibaya, ndiyo maana mradi umejengwa chini ya kiwango na wananchi wanaendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.

Kufuatia kuwepo kwa sakata hilo Mhandisi wa idara ya maji katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa ambaye alikuwa akisimamia ujenzi huo hivi sasa amesimamishwa kazi kwa ajili ya kupisha uchunguzi juu ya malalamiko hayo na kufuatia pia agizo lililotolewa na kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, baada ya kukataa kuufungua mradi huo alipokuwa katika kata hiyo ya Mkako wilayani humo.

Kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imetajwa kuwa ni ya Patty Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Kaimu Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Dkt. Patrick Banzi alithibitisha kusimamishwa kazi kwa Mhandisi huyo na kueleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo imeunda Kamati maalum ya watu saba ambao ni wataalamu wanaochunguza tuhuma hizo na mambo mengine yanayohusiana juu ya mradi huo na taarifa yake itatolewa baadaye mara itakapokamilisha kazi yake.

No comments: