Thursday, May 18, 2017

PAMS FOUNDATION WAFANIKIWA KUPUNGUZA MAUAJI YA TEMBO SELOU

Na Dustan Ndunguru, 
Songea.

SHIRIKA lisilokuwa la serikali, (PAMS Foundation) ambalo linajishughulisha na mapambano dhidi ya ujangili katika hifadhi ya pori la akiba la Selou, limefanikiwa kupunguza mauaji ya tembo kutoka mizoga 42 kwa mwezi hadi kufikia mzoga mmoja wa tembo baada ya miezi sita.

Pori hilo linaunganisha kati ya nchi mbili za Tanzania na Niassa Msumbiji ambapo shirika hilo lipo katika kukabiliana na uwindaji haramu unaofanywa na baadhi ya watu hapa nchini.

Akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa Mratibu wa shirika hilo, Maximillan Jenes alisema kuwa mafanikio hayo yametokana ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili, katika kuimarisha doria kwenye maeneo ya ushoroba wa Selou kwa upande wa Namtumbo mkoani Ruvuma, Nanyumbu mkoani Mtwara pamoja na hifadhi ya mto Ruvuma karibu na Msumbiji kwa kutumia ndege na magari.

Jenes alisema kuwa baada ya kuimarishwa kwa doria za anga katika hifadhi ya pori la akiba la Selou kwa upande wa Tanzania, vitendo hivyo vya ujangili hivi sasa vimeendelea kushamiri zaidi kwa upande wa pili wa mto Ruvuma ndani ya hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji ambapo hatua mbalimbali zinachukuliwa kwa kushirikiana kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kumaliza tatizo hilo.

Alizitaja sababu nyingine zilizosababisha kupungua kwa mauaji ya wanyama hao katika hifadhi hiyo kuwa ni kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wanyamapori, kuendelea kutoa elimu kwa jamii inayozunguka eneo hilo, kufadhili fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu pamoja na kutoa elimu ya kuwapenda wanyama katika shule za sekondari zinazozunguka eneo hilo.

Mratibu huyo alifafanua kuwa tangu shirika hilo lianze shughuli zake mnamo mwaka 2011 limeweza kuwanufaisha watu mbalimbali akiwemo mmoja wa mzawa kutoka katika jumuiya za jamii za hifadhi ya maliasili, kufuzu mafunzo na kuwa mkufunzi wa elimu ya kupambana na ujangili na kwamba mtumishi mwingine mzawa wa shirika hilo amepata mafunzo ya urubani ambapo kwa sasa anaendesha doria za anga.

Jenes alisema kuwa mtumishi mwingine mzawa wa shirika hilo amefanikiwa kuendesha mafunzo kwa makundi mbalimbali katika mikoa mingine juu ya namna ya kulinda mazao dhidi ya uharibifu wa tembo kwa kutumia uzio wa pilipili na kwamba mratibu wa mradi huo ameweza kutunukiwa tuzo ya mwaka kwa mhifadhi kijana itolewayo na International Union For Conservation of Nature (IUCN) na hivyo kumfanya kuwa mtanzania wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo na mmoja kati ya waafrika wachache waliowahi kutunukiwa.

Alisema kuwa shirika hilo pia limeanzisha mradi mdogo kwa ajili ya kupambana na wanyama waharibifu kwa lengo la kuzuia wasiweze kuwadhuru binadamu kwa kuwafukuza kwa kutumia ndege ndogo ambapo pia wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo wanayofanyia kazi jambo ambalo huwakwaza pindi wanapoendesha shughuli zao.

Mratibu huyo aliitaka jamii kushirikiana na shirika hilo katika kupambana na ujangili kwa madai kuwa wanyama wanapoongezeka kunavutia wawekezaji wengi kununua vitalu na kuiingizia serikali mapato yatakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kuboresha majengo ya zahanati, shule, barabara na miundombinu ya maji.



No comments: