Monday, May 1, 2017

MBUNGE WA JIMBO LA MBINGA MJINI SIXTUS MAPUNDA ATOA MSAADA WA BAISKELI KWA MLEMAVU ANAYETAMBAA KWA MIKONO NA MAGOTI

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo aliyesimama akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa kata ya Kitanda na baadhi ya wananchi waliokuwa wakishuhudia (ambao hawapo pichani) wakati wa makabidhiano ya baiskeli maalumu ya mlemavu Franko Tinda anayeishi katika kata hiyo, upande wa kushoto ni Diwani wa kata hiyo Zeno Mbunda na aliyekaa upande wa kulia ni Kaimu Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya mji wa Mbinga, Alphonce Njawa. 
Katibu wa Mbunge Jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo aliyevaa kofia akimkabidhi baiskeli maalumu (Wheel chair) mlemavu, Franko Tinda ambaye amekaa kwenye kiti. (Picha zote na Kassian Nyandindi) 
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, Sixtus Mapunda ametoa msaada wa baiskeli maalumu (Wheel chair) ya kutembelea mlemavu Franko Tinda (21) ambaye ni mkazi wa kata ya Kitanda wilayani humo yenye thamani ya shilingi 500,000.

Akikabidhi msaada huo mbele ya uongozi wa kata hiyo, Katibu wa Mbunge huyo Geddy Ndimbo alisema kuwa baiskeli hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na Mbunge Mapunda.

Ndimbo alisema kuwa jitihada hizo zilifanywa kwa lengo la kumsaidia Franko aweze kuondokana na taabu alizokuwa akizipata kwa kutambaa kwa mikono na magoti, hivyo aliona kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kuweza kumrahisishia asiendelee kupata adha hiyo. 

“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia uweze kutembea vizuri, nawaomba muendelee kumtunza vizuri mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana matatizo ya ulemavu tunapaswa kumjali na kumpatia ushirikiano wa kutosha pale anapohitaji msaada kutoka kwetu,

“Naomba pia hii baiskeli itunzwe vizuri itumike kwa matumizi yaliyokusudiwa kwani nina hakika sasa kitendo cha kumpatia hiki chombo tumeweza kumpunguzia adha alizokuwa anazipata hapo awali”, alisema Ndimbo.


Vilevile naye Kaimu Afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Alphonce Njawa alitoa rai kwa wananchi wa kata hiyo kwamba ni muhimu sasa wayatambue makundi maalumu kwa kuwajali na sio kuwatenga au kubagua kwa namna moja au nyingine.

Njawa alikemea tabia ya wazazi wasiwe wanawafanyia vitendo vya ukatili watu wenye ulemavu kama vile kuwafungia ndani kwani kufanya hivyo ni kuwanyima fursa muhimu ambazo wanapaswa kuzipata.

“Tusiwe tunawatenga hawa wenzetu kwa kuwafungia ndani, wazazi tukifanya hivi tutakuwa tunakosea hivyo tuwajali kwa kuwapatia haki sawa kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu tuache kuwanyanyapaa”, alisisitiza Njawa.

Pia kwa upande wake akitoa shukrani baada ya kupokea msaada huo mzazi wa mtoto huyo mlemavu, Michael Tinda alisema kuwa anamshukuru Mbunge huyo kwa kumpatia baiskeli hiyo ambapo alisema ni mkombozi mkubwa kwake kwani awali alikuwa akipata shida namna ya kutembea hasa nyakati za masika pale mvua zinaponyesha.

Alieleza kuwa wakati huo wa mvua walikuwa wakilazimika muda mwingi kumbeba mtoto huyo hivyo baada ya kupata baiskeli hiyo sasa ataweza kutembea vizuri bila kupata usumbufu wa aina yoyote ile.


Kadhalika Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake waliokuwa wamewasili wakati wa kupokea kiti hicho cha kutembelea mlemavu huyo alitoa shukrani kwa Mbunge huyo kuona umuhimu wa kumsaidia mtoto huyo, huku akiongeza kuwa msaada kama huo uendelee kutolewa kwa walemavu wengine pale panapojitokeza fursa ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kusaidia watu wenye ulemavu.

No comments: