Thursday, May 18, 2017

CHAMA CHA MAPINDUZI MKOANI RUVUMA CHASIKITIKA KUPOTEZA MADIWANI WAKE WILAYANI TUNDURU

Na Dustan Ndunguru, 
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimesema kwamba, kimepatwa na mshtuko mkubwa kufuatia kufariki dunia kwa Madiwani wake wawili kutoka katika kata za Lukumbule na Kalulu wilayani Tunduru mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Oddo Mwisho alisema vifo hivyo vilitokea Mei 13 mwaka huu na kuwaacha katika simanzi kubwa wananchi wa kata hizo.

Mwisho alisema diwani wa kata ya Lukumbule, Zubery Solo alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu na kwamba aliyekuwa diwani wa kata ya Kalulu Mnomba Kazembe amepoteza maisha baada ya kuvamiwa na watu wasiofahamika.

Alisema kuwa Chama hicho kimepoteza madiwani ambao walikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawatumikia wananchi wao kwa kutekeleza yale yaliyoainishwa ndani ya ilani yake na kwamba wananchi wa kata hizo wanapaswa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Wakati huo huo Mwisho alisema kuwa Chama cha mapinduzi kimekamilisha uchaguzi wake wa viongozi wa mashina kwa kata zote 184 za mkoa huo na kwamba kwa sasa wapo katika hatua za uchujaji wa majina ya wanachama walioomba uongozi katika ngazi ya jumuiya na matawi.

Mwisho alisema suala la rushwa halipaswi kupewa nafasi wakati huu ambao chama kinatafuta kuwapata viongozi wake ambao watakiongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, huku wakiwa na jukumu kubwa la kuhakikisha kinashinda katika chaguzi za dola na hivyo kuendelea kuongoza nchi.

Aliongeza kwa kuwataka wale wote waliozoea kupanga safu za uongozi kuacha tabia hizo kutokana na ukweli kwamba mabadiliko makubwa ya kikanuni na kikatiba yaliyofanywa ndani ya chama, kamwe hayaruhusu kuwepo kwa watu wenye nia ya kupanga safu na kwamba kwa wale ambao watabainika watachukuliwa hatua kali.





No comments: