Monday, May 8, 2017

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU AWATAKA WATENDAJI MJI WA MBINGA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA WANANCHI

Kiongozi Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour akiwasalimia wananchi (hawapo pichani) katikati ni Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya mji wa Mbinga Robert Mageni na upande wa kulia ni Meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (MBIUWASA) Patrick Ndunguru.
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

KIONGOZI Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour amewataka Watendaji waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wahakikishe kwamba, fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo ili ziweze kuleta tija katika jamii.

Aidha ameagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa kwa wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.

Hayo yalisemwa juzi na kiongozi huyo wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru wakati alipokuwa katika halmashauri ya mji huo akikagua jumla ya miradi kumi yenye thamani ya shilingi milioni 435,332,081 ambayo Mwenge huo umeweza kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa, kukaguliwa na kuzinduliwa.


Katika miradi hiyo amepongeza jitihada zilizofanywa za utekelezaji wake ambapo nguvu za wananchi zimetumika shilingi milioni 48,598,400 mchango wa halmashauri milioni 6,095,000 serikali kuu milioni 166,176,301 wadau wa maendeleo milioni 20,462,380 na watu binafsi ni shilingi milioni 194,000,000.

“Ni wajibu wenu watumishi wa umma kufanya kazi kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea na kulifanya taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo na wananchi waweze kuondokana na umaskini”, alisisitiza Amour.

Vilevile aliwataka watendaji hao wa serikali kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya vijana kufanya biashara na shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kukua kiuchumi.

Kadhalika alisisitiza kuwa vijana hao wahamasishwe pia kuunda vikundi vya ujasiriamali, ambavyo vitasajiliwa kisheria na kuweza kuwafanya waweze kukopesheka na taasisi za kifedha katika kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa risala ya utii wa wananchi wa halmashauri ya mji wa Mbinga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas Nshenye alisema kuwa tathmini ya mwaka 2016 inaonesha kuwa pato la mwananchi wa kawaida kwa mwaka katika halmashauri hiyo linakadiriwa kuwa ni shilingi milioni 1,500,000.

Lengo la Halmashauri hiyo alisema ni kuongeza pato hilo la sasa na kufikia milioni 2,500,000 ifikapo mwaka 2025 kutokana na wananchi wengi kuwa na mwitikio mkubwa wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Mwenge huo ambao umebeba ujumbe wa kitaifa (Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu) katika halmashauri ya mji wa Mbinga umeweza kupita kwenye miradi hiyo ambayo ni ya sekta ya elimu, afya, barabara, maji, kilimo, ufugaji nyuki, kiwanda cha kusindika unga wa mahindi pamoja na sekta ya mazingira upandaji miti na ujenzi wa nyumba bora ya kuishi mwananchi.


Hata hivyo katika risala hiyo Nshenye aliongeza kuwa kwa upande wa uwezeshaji wa vijana kiuchumi halmashauri katika mwaka wa fedha 2016/2017 imeweza kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani yenye jumla ya shilingi milioni 76,100,000 kwa ajili ya kuwezesha vijana katika shughuli za kukuza uchumi na kwamba tayari mpaka sasa imekwisha toa mikopo kwa vikundi vitano vya vijana yenye thamani ya shilingi milioni 6,000,000 ambavyo vinajishughulisha na kilimo na biashara mchangayiko.

No comments: