Monday, May 15, 2017

WAHAMIAJI HARAMU NANE WAKUTWA WAKIWA WAMEFARIKI DUNIA KATIKA MAKABURI YA KIJIJI CHA AMANI MAKOLO MBINGA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WATU nane wamekutwa wakiwa wamekufa na wengine 25 wakiwa hai katika eneo la makaburi ya kijiji cha Amani Makolo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambao inadaiwa kwamba walikuwa wakitoka nchini Ethiopia kwenda Afrika kusini kutafuta maisha.

Inadaiwa kuwa watu hao ni wahamiaji haramu ambapo walitelekezwa kwenye eneo hilo la makaburi, huku wakiwa na hali mbaya kutokana na kukosa chakula kwa muda mrefu hali ambayo ilisababisha wengine kufariki dunia.

Mmoja wa mashuhuda ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilibainishwa na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Salphire waliopo katika kijiji hicho, ambao walisikia sauti za watu wakiongea kutoka eneo hilo la makaburi na ndipo walipofuatilia waliona kundi la watu hao wakiwa wamelala chini.


Alisema kuwa baadaye wachimbaji hao waliamua kwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji cha Amani Makolo ambao nao walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wilayani Mbinga na kwamba baadaye walipokwenda katika eneo la tukio wakiwa wameongozana na mganga kutoka hospitali ya wilaya hiyo ndipo waligundua kuwa watu nane walikuwa wamekwisha fariki dunia na wengine wakiwa hai huku hali zao zikiwa taabani.

Alifafanua kuwa wachimbaji hao wadogo wa madini kwa kushirikiana na wanakijiji waliamua kuchangishana fedha na kuwanunulia chakula wahamiaji hao haramu ambao baada ya kupata chakula walianza kuongea kwa ufasaha kwamba walitokea Ethiopia ambapo waliingilia mpaka wa Namanga mkoani Arusha huku wakiwa wamepakiwa kwenye gari kubwa aina ya Lori na wao wakiwa wamepakiwa ndani ya kontena.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Dismas Kisusi alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alidai kuwa lilitokea Mei 14 mwaka huu majira ya usiku huko kwenye eneo la makaburi hayo ya kijiji cha Amani Makolo.

Kisusi alifafanua kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa wamebebwa kwenye Lori hilo ambalo lilikuwa na kontena ambamo ndimo walihifadhiwa wahamiaji hao ambao walikuwa wakisafiri kwenda Afrika kusini kupitia ziwa Nyasa.

Aliwataja  wahamiaji haramu nane waliofariki dunia kuwa ni Alado (19), Abeneth (20), Tashara Lile (18), Ammanuely Abana (20), Degu Abame (18), Manush Abama(19), Moconima Abama(17) na Gitacho Tamasger (19) ambao wote ni wanaume na kwamba wahamiaji wengine 25 wako hai na hali zao bado ni mbaya.


Kamanda huyo alisema kuwa uchunguzi utakapokamilika wahamiaji hao haramu watafikishwa Mahakamani kujibu mashtaka ya kuingia nchini bila kibali na kwamba aliwaasa wananchi kujenga tabia ya kutoa taarifa kwa jeshi hilo pindi wanapobaini kuwepo kwa watu wanaojihusisha na vitendo viovu ikiwemo uvamizi na watu wanaosafirisha wahamiaji haramu.

No comments: