Monday, May 1, 2017

BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAKE WA NNE

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limewafukuza kazi watumishi wake wa nne kutoka idara mbalimbali wilayani humo na wengine kupewa onyo kali baada ya kubainika kuwa na makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umma.

Akitoa taarifa hiyo ya kufukuzwa kazi watumishi hao katika kikao cha baraza hilo kilichoketi juzi kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Benward Komba alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kubainika kuwa wamekuwa na mazoea ya kufanya makosa hayo mara kwa mara. 

Komba aliwataja watumishi hao kuwa ni aliyekuwa afisa mtendaji wa kata ya Kitura, Daniel Komba ambaye amefukuzwa kazi kutokana na kufanya matendo kinyume na dhamira njema ambapo alifoji risiti za marejesho ya fedha shilingi 350,000 ambazo ni michango ya wananchi wa kata hiyo.


Alibainisha kuwa fedha hizo walikuwa wamechanga wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao ambapo alizitafuna kwa manufaa yake binafsi na halmashauri ilipofanya ufuatiliaji wa kina ilibaini kwamba risiti aliyoitumia kukusanyia fedha hizo haikuwa risiti halali ya serikali.

Vilevile aliwataja wengine kuwa ni Ramadhan Mang’una ambaye ni afisa kilimo msaidizi, Allan Ndunguru afisa mtendaji wa kijiji cha Ulima na Michael Nakitundu naye ni afisa mtendaji wa kijiji cha Ulolela ambao nao walishiriki kufanya ubadhirifu wa mali za umma katika vijiji hivyo.

Pia katika hatua nyingine baraza hilo la Madiwani lilitoa onyo kali kwa watumishi wengine wanne ambao nao walisimamishwa kazi na kufanyiwa uchunguzi wakituhumiwa kushiriki kufanya ubadhirifu wa mali za halmashauri hiyo na kubainika kwamba baada ya uchunguzi huo kukamilika hawakuwa na hatia hivyo wamerejeshwa kazini.

Watumishi hao walitajwa kuwa ni Sidney Mpangala ambaye ni mchumi kutoka idara ya mipango, David Davis afisa manunuzi, Onesmo Mapunda afisa mipango wa wilaya na Edward Kadege fundi sanifu idara ya ujenzi.


Hata hivyo awali waliposimamishwa kazi walikuwa wakituhumiwa kufanya ubadhirifu na wizi wa mali za umma katika kazi ya ujenzi wa kibanda cha mlinzi chenye thamani ya shilingi milioni 19,000,000 kwenye nyumba ya kuishi Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo ambayo imejengwa mtaa wa Kipika mjini hapa.

No comments: