Wednesday, May 17, 2017

MHANDISI IDARA YA MAJI MBINGA ASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI UJENZI MRADI WA MAJI

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mhandisi idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa kwa lengo la kupisha uchunguzi juu ya ujenzi wa mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako, ambao unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika ndani ya kata hiyo.

Vivian Mndolwa.
Aidha kusimamishwa kazi kwa Mhandisi huyo kunafuatia agizo lililotolewa Mei 8 mwaka huu na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour wakati anaukagua mradi huo ili Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aweze kuunda kamati itakayofanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo na baadaye hatua husika ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliouhujumu.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa Mhandisi huyo pia analalamikiwa akidaiwa kushindwa kusimamia kikamilifu taratibu za ujenzi wa mradi huo wa maji.

Mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa, lakini hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na fedha za mradi huo zimetumika katika kazi hiyo ya ujenzi.


Vilevile kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imeelezwa kuwa ni ya PATTY Interplan ya kutoka jijini Dar es Salaam na kwamba mkandarasi huyo ananyoshewa kidole kuwa anadaiwa kutokomea kusikojulikana na kuacha mafundi wake katika eneo la mradi bila kazi ya ujenzi huo kukamilika ipasavyo.

Mpaka sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo yamejengwa matenki mawili ya maji ikiwemo moja kubwa lenye ujazo wa lita 200,000 na lingine ndogo lenye ujazo wa lita 75,000 na ufukiaji chini wa mabomba ya Plastiki kutoka kwenye chanzo kikuu cha kuleta maji katika matenki hayo.

Kadhalika vituo 36 vya kuchotea maji vimejengwa lakini kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa mradi huo na kuleta maji kwenye mabomba hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa kata ya Mkako wilayani humo, inadaiwa kuwa siku kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru alipowasili hapo walipojaribu kuleta maji kwenye matenki hayo kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo hivyo vya kuchotea maji, mabomba hayo yalikuwa yamepasuka na kushindwa kuleta maji jambo ambalo linadhihirisha kuwa ujenzi wa mradi huo ni wa chini ya kiwango.

Hivyo basi, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga imeunda Kamati maalumu ya watu saba ambao ni wataalamu watakaoweza kuchunguza tuhuma hizo na mambo mengine yanayohusiana juu ya mradi huo.

Akizungumza na mwandishi wetu Kaimu Mkuu wa wilaya hiyo, Gilbert Simya alisema kuwa timu hiyo ya wataalamu ambayo imeundwa kuchunguza jambo hilo inatoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, Ofisi ya mkuu huyo wa wilaya na wengine ni wajumbe wa ngazi ya halmashauri ya wilaya.

Gilbert ambaye pia ni Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga alithibitisha kwa kusema kuwa kamati hiyo imeanza kufanya kazi rasmi Mei 12 mwaka huu na kwamba itakamilisha majukumu yake katika kipindi kisichozidi siku kumi.

“Msimamizi mkuu wa ule mradi ni Mhandisi mwenyewe wa maji wa wilaya, tunafanya kazi ya uchunguzi juu ya historia ya ule mradi namna ulivyotekelezwa na mwisho wa siku ukweli utakaopatikana kwa namna yoyote ile tutatoa taarifa ya mradi nini kinaendelea na hatua zipi zimechukuliwa katika jambo hili”, alisema.



No comments: