Monday, May 1, 2017

SHEREHE ZA MEI MOSI: RC RUVUMA APIGA MARUFUKU WAKUU WA IDARA KUZALISHA MADAI MAPYA YA UHAMISHO

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amewataka watumishi wa umma mkoani humo kuwa na subira juu ya madai yao wanayoidai serikali, kwani watalipwa mara baada ya kukamilika zoezi la uhakiki wa watumishi wake ambalo linalenga kuwabaini watumishi walioghushi vyeti na wale wasiokuwa na sifa ambao wanaliingizia taifa hasara kubwa.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amepiga marufuku tabia ya wakuu wa idara katika mkoa huo akiwataka kujiepusha kuzalisha madai mapya ya kuhamisha watumishi kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuwalipa stahiki zao.

Dkt. Mahenge alisisitiza kwamba uhamisho kwa mtumishi yeyote yule ufanyike mara baada ya kulipwa fedha zake za madai ya uhamisho, ili ziweze kumsaidia kuhama kutoka sehemu alipokuwa anafanyia kazi awali na kwenda sehemu nyingine hatua ambayo itasaidia kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Agizo hilo la Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge alilitoa leo wakati alipokuwa akihutubia mamia ya wafanyakazi wa serikali, taasisi mbalimbali, idara za serikali na sekta binafsi katika sherehe za siku ya Mei mosi zilizofanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.


Alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikisababisha chuki na uhasama kati ya mtumishi na viongozi wengine huku baadhi yao wakiichukia serikali yao, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya wananchi na moyo wa mtumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

“Kumuhamisha mtumishi pasipokuwa na fedha ya kumlipa sitaki kusikia tena, jambo hili halikubaliki mahali popote pale nawaonya wakuu wa idara na taasisi za umma zingatieni kanuni, sheria na taratibu mahali pa kazi”, alisisitiza Dkt. Mahenge.

Vilevile aliwataka watumishi kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi ikiwa ndiyo nguzo muhimu yenye kuleta ufanisi na kwamba waajiri na waajiriwa nao wanapaswa pia kutambua kuwa kila mmoja anayo haki yake katika utendaji wa kazi za kila siku.

Alisisitiza kuwa serikali haitafumbia macho kwa mwajiri yeyote atakayebainika kunyanyasa watumishi wake iwe ni mfanyakazi wa nyumbani, hotelini, shambani, baa na migodini badala yake kwa yule atakayekiuka taratibu husika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Pia alisema kuwa kila kiongozi ni lazima atende haki kwa kufuata sheria na taratibu na kanuni za kazi bila kuingilia majukumu ya mtu mwingine kwani uwepo wa migogoro sehemu za kazi hasa unyanyasaji watumishi, hupunguza ari ya kufanya kazi na matokeo yake ni kushuka kwa ufanisi wa kiutendaji katika taasisi husika.

Aliongeza kuwa wakati huu ambao serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kusimamia ufufuaji, uanzishaji na uimarishaji wa viwanda kila mfanyakazi kwa nafasi yake aliyonayo anatakiwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.

Dkt. Mahenge alieleza kuwa katika awamu hii Rais Dkt. Magufuli kupitia kauli mbiu yake ya Hapa kazi tu, amekuwa akisimamia kwa dhati uchumi wa nchi ya Tanzania uweze kukua kwa kuendelea kujenga viwanda vya aina mbalimbali vya kuzalisha mali ikiwemo viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa ambavyo vitasaidia kuongeza kipato na ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wao wafanyakazi ndani ya mkoa huo kupitia risala yao iliyosomwa na Theresia Tonya wameahidi kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa kuongeza juhudi maeneo yao ya kazi ili kuleta tija kwa lengo la kuharakisha ukuaji wa maendeleo hapa nchini.

Hata hivyo Tonya alisema wanaunga mkono hatua mbalimbali anazochukua Rais huyo hasa kwa watumishi wasiokuwa na sifa ambao wameajiriwa serikalini wamekuwa wakiibia serikali kwa njia ya kulipwa mishahara huku wakijua kwamba wanakiuka taratibu na sheria za utumishi wa umma.

  

No comments: