Wednesday, May 17, 2017

SAID MECK SADICK ATAJA SABABU ZILIZOMFANYA AACHIE NGAZI NAFASI YA MKUU WA MKOA


Na Mwandishi wetu,

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick amesema kuwa ameamua kuondoka serikalini baada ya kufanya kazi ya utumishi wa umma kwa muda mrefu na anakwenda kupumzika mkoani Mwanza, huku akiwa mfugaji wa samaki.

Aidha Sadick alisema kuwa pia kulingana na afya yake, anahitaji kupisha vijana wadogo wamsaidie Rais Dkt. John Pombe Magufuli kulingana na kasi yake kwani yeye ameepuka kumkwaza Rais wakati wa utekelezaji wa majukumu yake kama mkuu wa mkoa.

“Uamuzi huu wa kupumzika nilimuomba Rais kwa muda mrefu sana na nikirudi kijijini nitaendelea na ufugaji samaki maana nilishaandaa bwawa la kufugia, nitaendelea nalo huku nikiwaza jambo lingine la kufanya,” alisema.

Sadick alisema hayo jana wakati akitaja sababu zilizochangia kumuomba Rais Dkt. Magufuli kuacha kazi yake ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro.


“Namshukuru Rais kuridhia ombi langu, nimetumikia serikali tangu mwaka 1999 nikiwa mkuu wa wilaya na baadaye mkuu wa mkoa kuanzia mwaka 2005 hadi sasa ninapoondoka mwenyewe, nimeona ni wakati muafaka kumweleza aliyeniteua kuwa nahitaji kupumzika nikiwa na akili zangu timamu na afya njema,” alisema.

Alisema sababu nyingine kubwa ni kuhofia afya yake kutomudu kasi ya Rais Dkt. Magufuli, kwani alifanywa upasuaji mwaka 2012 na 2014 nchini India ingawa hakutaka kuweka wazi maradhi yaliyokuwa yakimkabili.

“Kama kiongozi muungwana lazima ifike mahali ukiri kwamba wapo vijana wenye uwezo mzuri na kasi ambayo inaendana na serikali ya awamu ya tano...........mimi nilishatekeleza wajibu wangu na mchango kwa serikali yangu, sasa inatosha, tupate mawazo na michango ya wengine”, alisema.

Sadick ambaye amekuwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro tangu Machi 13 mwaka 2016 alipoteuliwa na Rais Dkt. Magufuli, alisema siyo vibaya kwa kiongozi kujitathmini na kuwaachia wengine kama atabaini kasi yake ya utendaji kazi imeanza kupungua.


Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, Mkuu huyo wa mkoa Sadick pamoja na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebeisha Sheria Tanzania, Aloysius Mujulizi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Upendo Msuya waliomba kuacha kazi na Rais aliliridhia.

No comments: