Friday, May 5, 2017

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA AKATAA KUZINDUA MRADI BWALO LA CHAKULA MADABA SONGEA

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari St. Getruda katika halmashauri wilaya ya Madaba Songea mkoani Ruvuma wakiulaki Mwenge wa Uhuru, uliofika shuleni hapo kwa ajili ya kutoa ujumbe wa Mwenge kwa mwaka 2017 ambapo Kiongozi wa Mwenge  kitaifa, Amour Hamad Amour amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanaongeza bidii katika masomo yao ili waweze kufanikisha ndoto walizonazo  katika maisha yao.
Na Kassian Nyandindi,
Madaba.

MBIO za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu katika wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, zimeingia dosari kufuatia kiongozi wa mbio hizo, Amour Hamad Amour kukataa kuzindua mradi wa Bwalo la chakula shule ya msingi Lilondo iliyopo katika halmashauri ya wilaya hiyo.  

Kukataa kufunguliwa kwa mradi huo kumemfanya Mkuu wa wilaya hiyo, Pololet Kamando Mgema kujikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya Kiongozi huyo kumbana maswali magumu.

Aidha Amour alisema kuwa taarifa za ujenzi wa mradi huo alikuwa nazo tokea awali kabla ya kuwasili katika eneo la mradi, hivyo ana wasiwasi hata jengo hilo huenda likawa limebadilishwa matumizi yake.


“Tutoe mfano, hata kama leo hii Rais wa nchi anakuja kuufungua mradi huu katika wilaya yako unaweza kumleta katika mradi kama huu”, ? alihoji Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa.

Alisema kuwa hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa miradi mingi ambayo inaanzishwa katika wilaya ya Madaba, haichukuliwi hatua ya haraka katika kutoa huduma kwa walengwa.

Kadhalika kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Kamando Mgema alisikika akisema, “Mimi naomba nikiri mapungufu haya yaliyopo hapa, kwa sababu sikuwepo wakati mradi huu unajengwa”.

Pia Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, kukataa kufungua mradi huo alieleza kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango ukilinganisha na thamani halisi ya fedha iliyotumika katika kazi ya ujenzi wake shilingi milioni 19,460,000 huku taarifa za mradi huo nazo zikiwa zinakinzana.

Alieleza kuwa Mwenge wa Uhuru hauwezi kuzindua bwalo hilo ambalo thamani yake haiendani na kazi iliyofanyika hivyo kutakuwepo na utumiaji wa fedha ovyo kinyume na utaratibu husika.


Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari unathibitisha kuwa jengo hilo liliwekewa jiwe la msingi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu mwaka 2013 ambapo ndiyo ujenzi wake ulianza kufanyika.

No comments: