Friday, May 12, 2017

BOT YAIFUNGA RASMI BENKI YA WANANCHI MBINGA MAMIA YA WANANCHI WAKUSANYIKA WATAKA KUVAMIA ENEO LA BENKI

Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MAMIA ya Wananchi ambao ni baadhi ya wateja wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamekusanyika na kutaka kuvamia eneo la benki hiyo huku wakipaza sauti zao, wakidai akiba za fedha zao walizoweka baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchukua maamuzi ya kuifunga MCB na kusitisha shughuli zake zote za kibenki.

“Tunataka fedha, tunataka fedha sisi hatma ya fedha zetu ipo wapi kama leo hii benki inafungwa, tunataka fedha zetu”, walisikika wakisema kwa sauti kubwa.

Tukio hilo lilitokea leo Mei 12 mwaka huu majira ya asubuhi ambapo Askari wa kutuliza ghasia (FFU) ndiyo waliokuwa wamezunguka kulinda eneo la benki hiyo, wakati wafanyakazi wa BOT wakitangaza hadharani kufuta leseni ya biashara ya Benki ya Wananchi Mbinga kuanzia sasa.


Aidha benki kuu imeiweka MCB chini ya mfilisi na kuiteua Bodi ya bima ya amana kama mfilisi, kuanzia Mei 12 mwaka huu taarifa ambayo imetolewa na BOT leo asubuhi, imeeleza.

Uamuzi huu pia umechukuliwa baada ya benki kuu hapa nchini, kujiridhisha kuwa MCB inaupungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na taasisi za kifedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Kadhalika upungufu huo wa mtaji na ukwasi unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na kwamba kuendelea kwake kutoa huduma za kibenki kunahatarisha pia usalama wa amana za wateja hao.

Vilevile Benki Kuu ya Tanzania imeuhakikishia umma kwamba itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kutetea ustahimilivu katika sekta ya fedha.

BOT imechukua uamuzi huo wa kuifunga Benki ya Wananchi Mbinga kwa mujibu wa kifungu cha 56 (1) (g), 56 (2) (a), (b) na (d), 58 (2) (i), 11 (3) (j), 61 (1) na 41 (a) cha sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.

Hata hivyo Benki Kuu ya Tanzania imewataka wale wote wenye amana, wadai na wadaiwa wa iliyokuwa MCB kuwa wavumilivu wakati mfilisi kwa wakati muafaka atawafahamisha wenye amana, wadai na wadaiwa utaratibu wa malipo wa madai, ulipaji wa madeni na taratibu nyingine zitakazohitajika kwa mujibu wa sheria.



No comments: