Sunday, April 30, 2017

WANANCHI MBINGA WASISITIZWA JUU YA MATUMIZI YA KONDOMU

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, wakijadiliana jambo mara baada ya kuhitimisha kikao chao cha baraza la Madiwani kilichoketi juzi mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa kuwa na mazoea ya kutumia Kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Vilevile kutokana na maambukizi hayo kuendelea kushika kasi katika mji huo, halmashauri hiyo imejiwekea utaratibu wa kusambaza Kondomu hizo katika maeneo ya starehe na kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali namna ya kuepukana na maambukizi hayo.

Hayo yalisemwa juzi na Kaimu Afisa maendeleo ya jamii wa mji huo, Alphonce Njawa wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya Kamati ya kudhibiti ugonjwa wa ukimwi katika halmashauri hiyo.


Njawa alisema kuwa utekelezaji wa kazi za kitengo cha ukimwi, kinga na tiba kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu wameweza kufanya mikutano ya tahadhari juu ya mila na desturi potofu zinazochochea kuenea kwa maambukizi mapya ya ugonjwa huo hasa kwa watu waliokuwa kwenye ndoa.

Pia kwa ushirikiano na kitengo cha ustawi wa jamii elimu imetolewa kwa watu walio kwenye mahusiano ya ndoa ambao wanapeleka malalamiko yao mbalimbali juu ya unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa na waume zao ikiwemo utelekezwaji wa familia na wale wanaotaka kuachana wapatao 353 katika kipindi hicho wamepewa huduma hiyo.

“Kondomu pisi 864 zimetolewa kwa wanaume na wanawake katika kipindi hiki hasa kwa wale wanaokuja kuleta malalamiko ofisini, watu waliokuwa maofisini na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la boda boda sambamba na elimu juu ya matumizi sahihi ya kondomu hizo”, alisema Njawa.


Kadhalika kwa upande wao Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga walipongeza jitihada hizo zinazofanywa na kamati hiyo huku wakisisitiza kuwa ziendelezwe kwani ugonjwa huo umekuwa ukienea kwa kasi na kuendelea kutesa watu.

No comments: