Sunday, April 9, 2017

MANISPAA YA SONGEA KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAJI SAFI NA SALAMA

Na Julius Konala,      
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.325 katika mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji, kwa lengo la kuwafikishia wananchi wa Manispaa hiyo huduma ya maji safi na salama.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mhandisi wa maji wa Manispaa ya Songea, Samwel Sanya alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake kwa lengo la kuelezea utekelezaji mbalimbali wa miradi ya maji katika Manispaa hiyo.

Sanya alisema kuwa tangu mwaka 2007 halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza programu ya maji na usafi wa mazingira katika mitaa 10 ikwemo Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Muungano, Mahinya, Ngandula, Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa, Ruhila kati na Liwumbu.


Alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo bado unaendelea katika baadhi ya mitaa ambapo mitaa ya Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Muungano na Mahinya utekelezaji wake umekamilika huku akiitaja mitaa ambayo utekelezaji wake unaendelea kuwa ni Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa na Ruhila kati.

Alifafanua kuwa hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kila mtaa ni kama ifuatavyo ambapo Ruhuwiko kanisani umefikia asilimia 95 na utahudumia watu 3504, Mitendewawa asilimia 20 utahudumia watu 852 ambapo Ruhila kati umefikia asilimia 30 na kwamba utaweza kuhudumia watu 941.

Pia alieleza kwamba kulingana na mikataba yenye jumla ya kiasi cha shilingi biliioni 1.37 zinatakiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya maji kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji imeomba kuongezewa fedha kiasi cha shilingi milioni 107.344 ili ziweze kukidhi mahitaji ya ununuzi wa pampu 89 za maji.


Kadhalika aliongeza kuwa mpango wa matumizi ya fedha inayobaki kiasi cha shilingi milioni 187.655 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni kwa ajili ya kukarabati visima vya mikono katika mitaa 89 ambapo amedai kuwa tayari mzabuni wa ununuzi wa pampu hizo kwa ajili ya kuongeza utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 22,250 huku akidai kwamba jumla ya kiasi cha shilingi milioni 295 kitatumika kununulia pampu 89.

No comments: