Sunday, April 9, 2017

WADAU MBALIMBALI WATAKIWA KUCHANGIA UJENZI WA HOSPITALI NAMTUMBO

Na Kassian Nyandindi,      
Namtumbo.

KATIKA kuhakikisha kwamba huduma za tiba zinaendelea kuboreshwa, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imejiwekea mikakati ya kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo, ili ujenzi huo uweze kufanyika kwa urahisi.
Luckness Amlima.

Aidha kampeni ya uhamasishaji huo itafanyika kuanzia mwezi Julai mwaka huu na kwamba fedha zitakazopatikana, zitaweza kufanya kazi ya ujenzi wa majengo ya hospitali pamoja na kuimarisha miundombinu mingine katika sekta ya afya wakati ujenzi huo utakapofanyika.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi juu ya mikakati yake ya kukuza maendeleo katika sekta hiyo ya afya wilayani humo.

Amlima alisema kuwa wananchi waliopo ndani ya wilaya hiyo na nje ya wilaya anawaomba wajitokeze kwa wingi wakati kampeni hiyo itakapozinduliwa ili kuweza kufikia malengo ambayo wilaya imejiwekea katika kupambana na kufikia malengo ya ujenzi wa hospitali hiyo.


“Wilaya hii tokea ianzishwe hatuna hospitali hivyo kuna kila sababu sasa kwa sisi viongozi kuwa wabunifu katika kukabiliana na tatizo hili kwa vitendo ili katika sekta hii ya afya endapo tunafanikiwa kujenga hospitali yetu tuweze kuokoa vizazi vyetu”, alisema Amlima.

Vilevile akizungumzia kwa upande wa vituo vya afya na zahanati vilivyopo huko vijijini, alisisitiza kuwa serikali pia itaendelea kuboresha huduma husika hivyo anawaomba wananchi kuendelea kujitolea katika ujenzi wa majengo na miundombinu mingine mbalimbali ili kuweza kufikia malengo hayo.

Hata hivyo alisisitiza juu ya suala la wananchi kujitokeza kwa wingi na kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo kampeni hiyo itakapoanzishwa ndani ya wilaya ya Namtumbo, itakuwa inafahamika kwa jina la ‘Afya Kwanza’ na kwamba wadau wote watapewa taarifa ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kampeni hiyo.


No comments: