Saturday, April 15, 2017

MKUU WA WILAYA MBINGA AWATAKA WAKURUGENZI WAKE KUFUATILIA MAENDELEO YA WAKULIMA VIJIJINI

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MKURUGENZI wa halmashauri ya mji, Robert Mageni na wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito mkoani Ruvuma wametakiwa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya wakulima wa kahawa vijijini, ili waweze kujua ni matatizo gani wanakabiliana nayo katika uzalishaji na uendelezaji wa zao hilo na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.

Aidha maofisa ugani katika halmashauri hizo nao wamenyoshewa kidole wakilalamikiwa kwamba muda mwingi wamekuwa wakikaa maofisini kwa kutotembelea mara kwa mara wakulima hao kwa lengo la kuweza kuwapatia elimu namna ya uzalishaji bora wa zao hilo.

Hayo yalitokea juzi katika kikao cha wadau wa kahawa kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye aliwataka viongozi hao na maofisa kilimo kuhakikisha kwamba sasa wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa ikiwemo kwenda kwa wakulima vijijini kutatua matatizo katika sekta ya kilimo yanayowakabili.

“Nawataka Wakurugenzi wote wawili na maofisa kilimo simamieni na fuatilieni hili suala la maendeleo ya wakulima hawa ni lazima wapitieni huko waliko ili kuweza kujua wana matatizo gani yanayowakabili”, alisisitiza Nshenye.


Nshenye aliongeza pia wanapaswa wahamasishe wakulima hao wajiunge kwenye vikundi vya wakulima ili waweze kukopesheka kwa urahisi na hatimaye fedha za mikopo watakazopata, waweze kununua pembejeo za kilimo kwa kuendeleza mazao yao shambani na kuondokana na biashara haramu ya magoma ya kahawa ambayo huwafanya waendelee kuwa maskini.

Awali kwa mujibu wa taarifa ya uendelezaji wa zao la kahawa katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga ilielezwa kuwa halmashauri hiyo inampango wa kuongeza eneo la uzalishaji toka hekta 28,848 zilizopo sasa hadi kufikia hekta 31,554.6 ifikapo mwaka 2020.

Taarifa hiyo ambayo ilitolewa na Ofisa mazao wa wilaya hiyo, Deodatus Kissima alisema kuwa katika kufanikisha mpango huo halmashauri pia katika msimu wa mwaka 2017/2018 inatarajia kuzalisha miche 1,200,000 ya kahawa ikiwa ni miche itakayozalishwa na vikundi vya wakulima, makampuni na watu binafsi kwa njia ya vikonyo na mbegu.

Kissima alifafanua kuwa katika msimu wa mwaka huu halmashauri pia imepanga kukamilisha ujenzi wa mitambo ambayo ilikuwa haijaisha ujenzi wake ambapo imetenga fedha shilingi milioni 275,901,000 kumalizia ujenzi huo.

Vilevile kwa upande wa halmashauri ya mji wa Mbinga imejiwekea mikakati ya uendelezaji wa zao hilo kwa kuhakikisha kwamba wanaongeza uzalishaji kutoka hekta 7,458 hadi kufikia hekta 10,000 ifikapo mwaka 2020 ambapo mkakati huo utaenda sambamba na uzalishaji wa miche katika bustani mama 13 za kahawa ya vikonyo zilizopo sasa.


Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo Maganga Ngahy alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mikakati hiyo na kuongeza kuwa halmashauri itahakikisha inawawezesha wataalamu wa ugani kupita kutoa elimu kwa wakulima juu ya uboreshaji na utunzaji wa mashamba hususani kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo.

No comments: