Wednesday, April 26, 2017

MSHAWEJI: MSIKUBALI KUGAWANYWA KWA MISINGI YA DINI, KABILA AU ITIKADI ZA KISIASA

Na Muhidin Amri,     
Songea.

VIJANA katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameaswa wasikubali kugawanywa au kutumika kwa misingi ya dini, kabila au itikadi za kisiasa kwa maslahi ya watu wachache kwani kufanya hivyo watakuwa wana tenda dhambi kubwa kwa makundi mengine katika jamii ambayo inahitaji haki na usawa.

Aidha wametakiwa kuwa imara na kujitambua kutumia muda wao mwingi katika shughuli za kujiletea maendeleo, sambamba na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kukatisha ndoto za maisha yao ya baadaye.

Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na vijana hao kutoka kata za Manispaa hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya namna ya kutafuta njia bora katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao.


Alisema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo ni lazima wakatae kutumika na watu wenye tamaa ya madaraka ambao wanataka kuwatumia kama ngazi ya kufanikisha dhamira yao.

Mshaweji aliongeza kuwa badala yake vijana hao wanatakiwa kutumia nguvu zao katika kutafuta riziki ya maisha yao halali na endapo watafanya hivyo wataweza kuondokana na tabia ya kuwa omba omba.


Hata hivyo aliwaeleza kuwa katika kata ya Subira Manispaa ya Songea serikali imetenga eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda vidogo na vikubwa huku akiwataka vijana na wananchi wenye uwezo wa kifedha kuchangamkia fursa hiyo kupata maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uwekezaji huo.

No comments: