Monday, April 10, 2017

SERIKALI YALALAMIKIWA KWA KUTOIFANYIA UKARABATI SHULE KONGWE YA SEKONDARI KIGONSERA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

WANAFUNZI wa shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia serikali kwa kutoifanyia ukarabati shule hiyo kwa muda mrefu kutokana na majengo yake kuwa chakavu jambo ambalo linahatarisha hata usalama wao.

Aidha walisema kuwa majengo mengi yakiwemo mabweni ya kulala wanafunzi hao, vyumba vya madarasa ya kusomea pamoja na vyoo yapo katika hali mbaya na kwamba kuna kila sababu sasa kwa serikali kuchukua hatua juu ya namna ya kuyafanyia ukarabati ili waweze kuondokana na adha hiyo.

Malalamiko hayo yalitolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, katika mahafali yao ya 18 ya wahitimu kidato cha sita yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani hapa.

Salum Hassan ambaye ni mwanafunzi anayetarajia kuhitimu mwaka huu alisema kuwa katika kipindi chote cha miaka miwili ambayo yeye na wenzake wameishi shuleni hapo, wamekuwa wakikumbana na adha hiyo huku wakati mwingine wakihofia hata kuangukiwa na majengo ya shule hayo kutokana na uchakavu uliopo.


“Majengo haya tokea yajengwe miaka ya sitini hayajafanyiwa ukarabati viongozi wengi wamekuwa wakitembelea shuleni hapa na kujionea namna majengo yalivyochakaa lakini hakuna hatua tunayoweza kuiona ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa kweli inasikitisha sana”, alisema Hassan.

Emmanuel Sanga, David Mhande na Vamentine Wella nao walieleza kuwa wakati umefika sasa kwa wale viongozi wenye dhamana ya kusimamia masuala ya elimu hapa nchini, wahakikishe wanaiangalia shule ya sekondari Kigonsera kwa jicho la huruma kwani shule hiyo ni kongwe na ambayo viongozi wengi wamesoma hapo akiwemo Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa kuhakikisha inafanyiwa ukarabati huo ili iweze kuendelea kudumu miaka mingi ijayo kwa faida hata ya kizazi cha sasa na baadaye.

Walifafanua kuwa endapo kama hakuna hatua zitakazoweza kuchukuliwa kwa haraka katika kunusuru hali hiyo kuna uwezekano mkubwa ukafika wakati shule hiyo ikafungwa na watoto wakarudishwa majumbani kwao kutokana na uchakavu huo wa majengo.

“Hali ya shule yetu siyo nzuri kabisa ni vyema serikali ikaipatia kipaumbele kwa kuifanyia ukarabati wa hali ya juu ili kudumisha usalama wa wanafunzi wanaosoma hapa shuleni”, walisema.

Awali Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Jema Yohana katika taarifa yake alimweleza mgeni rasmi wa mahafali hayo ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kuwa shule ya sekondari Kigonsera yenye kidato cha tano na sita ina jumla ya wanafunzi 850 ambapo wanafunzi wa kidato cha sita ni 432 na kidato cha tano ni 418 na kwamba imekuwa ikiendelea kufanya vizuri katika nyanja ya taaluma kwa kupiga hatua mbele kila mwaka na kujiwekea mkakati wa kufuta daraja sifuri.

Jema alibainisha kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa ni kihunzi katika kufikia malengo yaliyowekwa ambapo alizitaja changamoto hizo kuwa ni uchakavu huo wa miundombinu ya majengo, upungufu wa nyumba za watumishi, ubovu wa barabara iingiayo kwenda shuleni pamoja na daraja, uchakavu wa magari na ukosefu wa baadhi ya watumishi wa kada mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema kuwa changamoto zinazoikabili shule hiyo zitafanyiwa kazi na serikali na kuwataka wataalamu wa majengo kwenda shuleni hapo kuangalia namna miundombinu ilivyochakaa ili hatimaye gharama halisi ya ukarabati iweze kufahamika na hatua zichukuliwe.

Pia Nshenye aliwaasa wahitimu wa kidato cha sita kwa kipindi watakachokuwepo majumbani kwao wasijiingize na makundi maovu ambapo kwa kufanya hivyo kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kufuta ndoto zao za kujiendeleza kimasomo.


Pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa hivi sasa wanapaswa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na sio kupoteza muda mwingi kukaa vijiweni bila kazi muhimu ya kufanya na kwamba, inafaa pia wafahamu duniani kote kuna tatizo la ukosefu wa ajira hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo wahakikishe kwa wale ambao watapata fursa ya kujiunga hata kwenye vyuo vya ufundi wasipuuze kwani ni moja kati ya sekta ambayo imekuwa ikiwafundisha vijana fani mbalimbali ambazo ni rahisi kujiajiri.

No comments: