Sunday, April 23, 2017

TCB YAWAPIGA JEKI WAKULIMA WA KAHAWA

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

MWENYEKITI wa Mfuko wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Hyasint Ndunguru amesema kuwa bodi hiyo hapa nchini, imetoa shilingi milioni 40 kwa ajili ya kugharimia nusu ya bei ya miche bora ya kahawa kwa wakulima.

Ndunguru alisema kuwa gharama hiyo imelipwa kwa Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) ambao ndiyo wanaozalisha miche hiyo kwa gharama ya shilingi 300 kwa kila mche mmoja wa kahawa.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo katika kikao cha Wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma kilichofanyika mjini Songea kwenye ukumbi wa Hanga, ambapo wadau hao walikutana kwa lengo la kuhamasishana namna ya kudumisha ubora wa zao la kahawa mkoani hapa. 


“TaCRI tumekwisha walipa nusu ya bei ya kila mche wa kahawa shilingi 150 hivyo mkulima atakapokwenda kununua mche wa kahawa kwenye kituo cha taasisi hii popote pale kilipo anapaswa kulipia nusu nyingine ya bei ambayo ni shilingi 150 tu kwa mche mmoja na sio vinginevyo”, alisema Ndunguru.

Alisema kuwa hayo yote yanafanyika kufuatia maazimio yaliyowekwa na wadau wa kahawa ambayo yalipitishwa kitaifa katika vikao husika kwamba asilimia 0.75 ya ushuru wa fedha yote inayopatikana kwenye minada ya kahawa itumike kuisaidia serikali kwa shughuli za utafiti.

Vilevile aliongeza kuwa asilimia 0.2 imekuwa ikisaidia gharama za uendeshaji katika shughuli za minada hiyo na kwamba kufuatia maazimio hayo mfuko umeweza kupata hati safi kutokana na utendaji mzuri wa maazimio ya wadau hao.   

Kwa upande wao wadau wa zao hilo walipokuwa wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika kikao hicho waliweka maazimio kwamba Bodi ya kahawa Tanzania vilevile ikae na halmashauri za wilaya na kukubaliana kutumia takwimu za uzalishaji wa kahawa za halmashauri husika katika ukokotoaji wa hesabu za ushuru wa makato ya kahawa mnadani Moshi.

Pia walieleza kuwa bodi hiyo inapaswa itoe hati ya makato hayo na kurejesha ushuru uliokatwa kwenye halmashauri hizo kwa wakati kwa kuzingatia taratibu za mikataba husika.


Kadhalika naye Meneja wa TCB Kanda ya Ruvuma, Peter Bubelwa aliwaeleza wadau hao kuwa ili kuongeza thamani ya ubora wa kahawa kuna kila sababu sasa kwa wakulima kuendelea kuwahamasisha pia watumie mashine za CPU ambazo huongeza ubora wakati wa ukoboaji wa kahawa mbivu kipindi cha msimu wa mavuno ya zao hilo.

No comments: