Wednesday, April 5, 2017

WASHIRIKI MANUNUZI YA UMMA WATAKIWA KULETA MABADILIKO CHANYA


Na Kassian Nyandindi,      
Mbeya.

WAANDISHI wa habari Nyanda za juu kusini ambao wameshiriki kwenye mafunzo ya namna ya kuandika habari za manunuzi ya umma, wametakiwa huko waendako wakafanye kazi kwa weledi na kuleta mabadiliko chanya kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha imeelezwa kuwa wanapaswa kazi zao kuzifanyia uchunguzi wa kina kabla ya kuujulisha umma ili ziweze kuleta tija na kwamba kipengele cha habari za manunuzi kimekuwa na ombwe kubwa ambalo linahitaji kuzibwa kwa kuandika habari hizo kwa uwazi na ukweli.

Hayo yalisemwa na Monica Malikita ambaye ni Mkufunzi wa mafunzo ya uandishi wa habari za manunuzi ya umma (PPRA) kutoka Kanda ya Dodoma, ambayo yaliwakutanisha waandishi hao kwa siku tatu na kufanyika kwenye ukumbi wa Mkapa Jijijini Mbeya.


“Tunataka kuona huko muendako mnakwenda kuripoti habari za manunuzi kwa weledi na mnaendelea kuujulisha umma kinagaubaga kwa kila jambo litakalokuwa linatokea katika vipengele vya manunuzi ya umma, hasa kwenye halmashauri za wilaya ambako ndiko shughuli za manunuzi zimekuwa zikifanyika mara kwa mara”, alisema Malikita.

Naye Castor Komba ambaye ni Mkufunzi wa mafunzo hayo aliongeza kuwa lengo la mada walizofundishwa waandishi hao ni kuwafanya pia waweze kuelewa sheria za manunuzi hayo na marekebisho yake, ikiwemo masuala ya usimamizi wa mikataba na uhalisia wa thamani ya fedha iliyotumika kwenye mradi husika.

Komba aliongeza kuwa sheria mama ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 baadhi ya vipengele vimekuwa vikisisitiza na kutoa maelekezo kwa watendaji husika katika taasisi za umma kufanya kazi kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa na sio vinginevyo.
Alifafanua kuwa kwa upande wa halmashauri za wilaya, siku zote msimamizi Mkuu wa manunuzi ya umma ni Mkaguzi wa ndani (Internal Auditor) hivyo kazi yake kubwa anapaswa kuhakikisha kwamba taratibu za manunuzi zinazingatiwa wakati wote bila kufanyika au kuwepo kwa ukiukwaji wa aina yoyote ile.


Hata hivyo naye Henry Muhanika ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) alisisitiza pia umefika wakati sasa kwa wanahabari wote Tanzania, kuondoa hofu na uoga katika utendaji wa kazi zao za kila siku hasa pale wanapofikia hatua ya kuibua mambo ambayo yanalenga kuinufaisha jamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: