Saturday, April 15, 2017

DC MBINGA APIGA MARUFUKU MAKAMPUNI KUHIFADHI KAHAWA KWENYE MATURUBAI

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akihutubia katika mkutano wa wadau wa kahawa uliofanyika juzi mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MAKAMPUNI yanayonunua zao la kahawa katika halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma yamepigwa marufuku kuhifadhi zao hilo kwa kutumia maturubai, badala yake wanapaswa kuhifadhi kwenye maghala ili kuweza kudhibiti ubora wake.

Vilevile agizo limetolewa kwamba ili kuweza kuendelea kuongeza ubora wakati wa mavuno ya zao hilo, makampuni hayo yanapaswa kukoboa kahawa kwa kutumia mashine za CPU’S kuliko kuwaachia wakulima wakoboe majumbani kwa njia ya kawaida.

Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha wadau wa kahawa ambacho kiliketi mjini hapa kwa lengo la kujenga mikakati ya uendelezaji wa zao hilo.

“Sisi kama viongozi tutaendelea kusimamia sheria za kilimo cha zao hili nawataka pia makampuni yote yanayonunua kahawa jengeni ushirikiano na serikali tuweze kuwa pamoja, sote tunaamini wafanyabiashara na serikali tukiwa pamoja ndiyo tunaweza kuendesha maendeleo ndani ya nchi yetu”, alisema.

Kadhalika aliongeza kuwa kwa makampuni, vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima ambavyo vitaonekana kufanya vibaya kwa kukiuka taratibu na sheria ameapa kwamba atavifutia usajili wake.


Alisema kuwa kuendelea kuviacha huku vikionekana wazi kuumiza wakulima itakuwa sio busara, bali dawa yake ni kuvifuta kwani vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kumzorotesha mkulima bila uwepo wa sababu yoyote ile ya msingi.

Vilevile alisisitiza kuwa kwa makampuni ambayo hayajalipa malipo yake ya pili msimu wa mavuno ya kahawa mwaka jana kwa mkulima ni lazima wakalipe, vinginevyo atahakikisha anayachukulia pia hatua kali za kisheria.

Naye kwa upande wake Meneja mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Kanda ya Ruvuma, Peter Bubelwa alisisitiza makampuni hayo kuzingatia sheria zilizowekwa ikiwemo kila kampuni kuwa na leseni inayomruhusu kununua zao hilo wakati wa msimu wa mavuno.

Pia alizungumzia juu ya ubora wa kahawa ambapo Bubelwa alisema kuwa endapo tunahitaji ongezeko la uzalishaji wa zao hilo itakuwa ni ndoto kama miti iliyozeeka huko shambani kwa mkulima, haitaboreshwa ipasavyo hivyo wataalamu husika wanapaswa kuendelea kwenda vijijini kuelimisha wakulima hao kwa kuwapatia elimu namna ya kuzingatia kanuni za kilimo bora.

Aliongeza kuwa katika msimu wa mavuno mwaka huu mkoa wa Ruvuma umejiwekea lengo la kufikia tani 18,000 za uzalishaji wa kahawa.

Pamoja na mambo mengine kwa upande wao wadau wa kahawa wilayani Mbinga nao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na serikali hivyo walishauri taasisi za fedha kama vile benki, nazo zione umuhimu wa kumsaidia mkulima wa zao hilo kwa kumkopesha fedha kwa masharti nafuu atakayoweza kununua pembejeo za kuendeleza zao la kahawa.

Akichangia hoja katika kikao hicho mmoja kati ya wadau hao, Mario Millinga alisema kuwa umefika wakati sasa mkulima huyo pia anapaswa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili aweze pia kuachana na ugumu wa maisha anayokabiliana nayo sasa kule kijijini mara baada ya kuuza mazao yake shambani.


Millinga alisisitiza kuwa endapo mkulima huyo atakuwa na tabia ya kuweka akiba ya fedha zake za mauzo ya kahawa kwa kila msimu wa mavuno itakuwa rahisi kwake kununua pembejeo zitakazoweza kuboresha mashamba yake hatimaye kuweza kuondokana na ugumu huo wa maisha.

No comments: