Sunday, April 16, 2017

DC MBINGA KUWACHUKULIA HATUA WATAKAOKIUKA AMRI HALALI KATIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA NGURUWE

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ametoa amri ya kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaokiuka amri halali ya kupambana na ugonjwa wa homa ya nguruwe, African Swine Fever ambao umeingia katika halmashauri ya wilaya hiyo.
Cosmas Nshenye.

Aidha ugonjwa huo ambao umeingia katika kata ya Kitura na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji wa wanyama hao, ambapo nguruwe 18 wamekufa na hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa ili usiweze kusambaa katika maeneo mengine jirani na kuleta hasara zaidi.

Nshenye ametoa amri hiyo kupitia nakala yake ya barua ya Aprili 10 mwaka huu yenye kumbukumbu namba AB. 120/475/01/18 iliyosambazwa kwa viongozi wa wilaya hiyo ambayo mwandishi wetu anayo nakala yake ikisisitiza juu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Mimi Mkuu wa wilaya hii kwa mujibu wa sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na sheria ya magonjwa ya mifugo natoa amri ya kuwachukulia hatua wale wote watakaoshindwa kufuata maelekezo, amri, zuio na katazo hili ambalo limetolewa kisheria chini ya mamlaka halali ya sheria kifungu cha 62 – 1 cha masharti ya karantini dhidi ya ugonjwa wa homa ya nguruwe”, alisema Nshenye.


Nshenye alisema kuwa kufuatia amri hiyo kwa wale wote watakaokiuka utaratibu huo watatozwa faini ya shilingi 300,000 na isiyozidi 500,000 au kushtakiwa mahakamani na kwenda jela kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.

Alisema kuwa amri hiyo ni pamoja na kuzuia kutoa au kuingiza nguruwe pamoja na mazao yake kama vile nyama na mbolea katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga bila idhini ya Daktari wa mifugo aliyeidhinishwa.

Pia alieleza kuwa wanapaswa wafugaji wote kuanza sasa kunyunyiza dawa katika maeneo yote ya ufugaji ambao mabanda yao yamepata ugonjwa huo, ili kuweza kuangamiza vimelea vya ugonjwa na wafugaji wajenge mabanda hayo vizuri ili kuzuia kuzurula wanyama hao hovyo mitaani.

Kwa upande wake naye Daktari wa mifugo wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Dkt. Patrick Banzi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ugonjwa wa African Swine Fever huenea kwa kulisha nguruwe masalia ya nyama ya nguruwe mwenye ugonjwa, maji, majani, chakula, na mtu ambaye amevaa buti ambazo zimekanyaga kutoka eneo la mabanda ambayo yana ugonjwa.

Vilevile nguruwe mwenye homa kugusana na nguruwe ambaye hana ugonjwa na pia husambazwa na wadudu warukao au wang’atao kama vile kupe.

Kadhalika alifafanua pia dalili za ugonjwa huo kwa mnyama huyo kuwa ni pamoja na  nguruwe wagonjwa kujitenga na wenzao, kunyongeka, kukosa hamu ya kula, kupenda kukaa muda mwingi kwenye kivuli, kujikusanya pamoja, kuhema kwa shida na kwa wale wenye ngozi nyeupe ngozi yao kuwa nyekundu hasa maeneo ya chini na miguu.


Dkt. Banzi alieleza dalili zingine kuwa ni wengine huwa wanaharisha damu, hupata mafua au kutoa mate yenye povu povu ambayo huwa na damu na kutapika, miguu ya nyuma kukosa nguvu na kuwa dhaifu na hukaa kama mbwa.

No comments: