Monday, April 10, 2017

GAMA AVIMWAGIA MAMILIONI VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI MANISPAA YA SONGEA

Na Julius Konala,   
Songea.

MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama ametoa mkopo wa shilingi milioni 13 kwa ajili ya vikundi mbalimbali 26 vya ujasiriamali jimboni humo, kwa lengo la kuvisaidia kukua kiuchumi ili waweze kuondokana na umaskini.

Akikabidhi hundi hizo mwishoni mwa wiki kwa viongozi wa vikundi vya ujasiriamali kwa niaba ya Mbunge huyo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea, Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema amewataka wajasiriamali hao kutumia mikopo hiyo kwa kazi iliyokusudiwa.

Mgema aliwaonya wajasiriamali hao kuacha tabia ya kutumia fedha hizo kwa mambo ya anasa ikwemo kwenye mambo ya ulevi, mashindano ya kuvaa nguo pamoja na kucheza mchezo wa kupeana jambo ambalo alidai kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha wakashindwa kurejesha mkopo huo kwa wakati.


Aidha alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo, Gama kwa kutoa mkopo huo kwa vikundi hivyo vya ujasiriamali kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwaongezea safari ya kukuza mitaji yao na kuwainua kiuchumi katika shughuli zao za kimaendeleo.

Naye Katibu wa Mbunge huyo, Kassian Mbawala alisema kuwa lengo la Mbunge huyo ni kutoa mikopo hiyo kwa vikundi vya ujasiriamali na kutaka kuviwezesha ili viweze kujiinua kiuchumi ikizingatiwa kwamba mkoa wa Ruvuma, upo nyuma kimaendeleo kwa kuwa na viwanda ambapo amedai kuwa  kila kikundi kitanufaika na mkopo huo kwa kupewa shilingi 500,000.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya hundi hizo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini, Gerlod Mhenga alidai kuwa kitendo kilichofanywa na Gama ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na ahadi aliyoitoa katika kampeni zake wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji akizungumza katika hafla hiyo ameishukuru ofisi ya Mbunge kwa kutoa mkopo huo kupitia mfuko wa jimbo na kwamba amewataka wajasiriamali hao kuutumia vizuri ili waweze kupiga hatua mbele na kuelekea katika malengo yao ya kuunda SACCOS yao.


Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mkopo huo Anna Mlimila na Mohamed Gayo wamemshukuru Mbunge huyo kwa mkopo alioutoa huku wakiahidi kuutumia vizuri kwa kazi na malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kwa ajili ya kukuza mitaji yao.

No comments: