Friday, April 7, 2017

MLETE KATA YA TANGA SONGEA WAHAMASIKA KUTUMIA MBEGU YA PANNER

Ofisa masoko wa Kampuni ya Pannar Seed Tanzania Limited, Sabasaba Manase upande wa kulia akiwaonesha juzi wakulima wa kijiji cha Mletele katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma shamba lililotumia mbegu aina ya Pannar 15 za mahindi ambazo zinasambazwa na kampuni hiyo ambapo mbegu hizo zinatajwa kuleta mafanikio makubwa kwa wakulima kutokana na kukomaa haraka na hata kuhimili vizuri hali ya hewa.
Na Julius Konala,    
Songea.

BAADHI ya wakulima wanaoishi katika maeneo ya Mletele kata ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wataondokana na tatizo la njaa baada ya kuhamasika kutumia mbegu ya mahindi ya muda mfupi aina ya Panner 15 msimu wa kilimo wa mwaka jana, ambapo mbegu hiyo imeonesha mafanikio makubwa katika ongezeko la mavuno.

Hayo yalisemwa jana wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti mjini hapa, mara baada ya kutembelea katika kata hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za kilimo zilizofanywa na wakulima hao.

Waliyataja mafanikio mengine yaliyotokana na mbegu hiyo kwamba inao uwezo wa kuhimili ukame na magonjwa mbalimbali ya kutu ya majani, jambo ambalo walidai kuwa limewafanya wahamasike kupanua ukubwa wa mashamba yao na kutumia mbegu hiyo ya Panner katika msimu ujao wa kilimo.


Mmoja wa mashuhuda waliotumia mbegu hiyo Said Kajanja, Erasto Makoti na Ania Nkilima wote wakazi wa Mlete wameipongeza kampuni ya Panner kwa kutoa elimu ya matumizi bora ya mbegu kwa wakulima hao.

Walisema kuwa elimu waliyoipata imechangia kuongeza tija katika kilimo cha mahindi hali iliyowafanya waweze kuondokana na baa la njaa, kumudu gharama za kusomesha watoto wao, kujiwekea akiba ya chakula na kujenga nyumba bora ikilinganishwa na kilimo cha zamani ambacho hakikuwa na tija kwao.

Kwa upande wake Ofisa masoko wa kampuni ya Panner Nyanda za juu kusini Sabasaba Manase alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kampuni yake iliamua kufanya utafiti kwa ajili ya kutumia mbegu hiyo kwa lengo la kukabiliana na ukame na baa la njaa pindi inapotokea.

Manase alisema kuwa sifa nyingine ya mbegu hiyo mazao yanapokauka yanainama chini kiasi kwamba mvua inaponyesha hayawezi kuharibika, majani yake yanafunga na mbegu yake inatoa magunia 35 ya mahindi kwa ekari moja hivyo amewashauri wakulima hao kutumia mbegu hizo kipindi cha hali ya hewa kinapokuwa kibaya.


Pia aliongeza kuwa lengo la kampuni ya Panner ni kuwafikishia elimu ya shamba darasa wakulima hao ili waweze kutoka kwenye kilimo cha kawaida na kuwapeleka katika kilimo cha biashara, ili waweze kusomesha vijana wao na kujenga nyumba bora huku akidai kuwa mpango wa kampuni kwa siku za mbele ni kuwafanya wakulima waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusaga mahindi na kuuza unga.

No comments: