Friday, April 14, 2017

HDT WAFANIKIWA KUWARUDISHA WALIOPOTEA KUMEZA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI WILAYANI MBINGA

Ofisa unasihi na upimaji wa shirika la Health Promotion Tanzania (HDT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Zawadi Mtambo.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT) lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) limefanikiwa kuwarudisha watu 1,229 ambao walipotea kumeza dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo na kuwarudisha katika Vituo vya tiba (CTC) kwa ajili ya kupata huduma endelevu.

Aidha kati ya hao taarifa za awali zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 717 waliopotea ambapo HDT walifanikiwa kuwarudisha wagonjwa 507 ambao sasa wanaendelea kumeza dawa hizo.

Kadhalika katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu kulikuwa na wagonjwa 1,684 waliopotea na sasa wamerudishwa wagonjwa 722 hivyo zoezi hilo utekelezaji wake umefikia asilimia 42.9 ambapo malengo ya shirika katika utekelezaji huo ni kufikia asilimia 80 na kwamba kazi hiyo bado inaendelea.


Dkt. Joachim Henjewele ambaye ni Meneja Mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT) lililopo Mbinga mjini, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya ya VVU alisema hayo juzi wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake.

Dkt. Henjewele alisema kuwa shirika hilo lilikuja Mbinga kwa sababu ya kuwa na taarifa za awali kwamba kuna maambukizi makubwa ya virusi vya ugonjwa huo ambapo hivi sasa wamekuwa wakiendelea na zoezi la upimaji wa hiari.

Naye Ofisa unasihi na upimaji wa shirika hilo, Zawadi Mtambo aliongeza kuwa pia wamekuwa wakijishughulisha na utoaji wa kinga kwa jamii, utoaji wa tiba na elimu dhidi ya magonjwa ya zinaa, kaswende, kasonono pamoja na mila potofu ambazo zinasababisha kupata maambukizi ya VVU.


Pamoja na mambo mengine Ofisa huyo alieleza pia HDT wamekuwa wakipinga masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, elimu ya lishe imekuwa ikitolewa kwa watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi pamoja na elimu ya kujikwamua kiuchumi kwa makundi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo.

No comments: