Wednesday, April 26, 2017

WAAJIRI WATAKIWA KUHAKIKISHA MITAMBO NA VIFAA VYA KAZI VINAFANYIWA UKAGUZI MARA KWA MARA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde akitoa hotuba yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi uliofanyika Aprili 25 mwaka huu mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mara baada ya kumaliza mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.     (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma)
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

SERIKALI imewataka waajiri wote na wadau kwa ujumla hapa nchini kuhakikisha kwamba maeneo au sehemu za kazi, mitambo na vifaa vya kufanyia kazi vinafanyiwa ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa havileti madhara kwa wafanyakazi.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

“Kwa upande wa Serikali jukumu letu kubwa ni kuweka na kusimamia sera ya Usalama na Afya mahali pa Kazi, kutunga na kusimamia sheria za usalama na afya mahali pa Kazi na kuweka viwango mbalimbali vya usalama na afya sehemu za kazi” alisisitiza Mavunde.

Mavunde alisema kuwa kwa sasa kanuni ya kuripoti ajali na magonjwa imekamilika na kuanza kutumika tangu mwezi Septemba, mwaka 2016.

Ambapo ameshauri wafanyakazi kuwasaidia waajiri wao kusimamia mifumo iliyopo, kujilinda wao binafsi ili wasiumie ama wasipate magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na kutumia ipasavyo vifaa vyote vya kujikinga wanapokuwa kazini.

Mavunde alisema kuwa serikali inaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, hivyo bado kuna changamoto ya kupata taarifa kuhusu ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hii inatokana na waajiri wengi kutoripoti taarifa hizo kama sheria inavyoelekeza.

Kwa mantiki hiyo Serikali inaandaa mfumo ambao utaongea na mifumo mingine ili kupata taarifa za ajali na magonjwa.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA) imejipanga kuhakikisha kuwa usalama na afya za wafanyakazi hao zinalindwa kwa kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia taratibu zote za usalama na afya kwa mujibu wa sheria na 5 ya Mwaka 2003, ili kulinda nguvu kazi ya taifa hili”.

Aidha Aprili 28 kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwakumbuka wahanga wa majanga yanayotokea sehemu za kazi.

Madhumuni makubwa ya kuadhimisha siku hii ni kuendesha kampeni ya kimataifa ya kuboresha usalama na afya kazini na kuhamasisha utengenezaji ajira zenye staha.

Pia kuhamasisha waajiri na wafanyakazi na umma kwa ujumla kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi yanapungua au kutotokea kabisa sehemu za kazi.

Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajia kufanyika Moshi mkoani Kilimanjaro kwa kujumuisha shughuli hizo kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 ambapo yatatanguliwa na kongamano la wadau wa usalama na afya.



No comments: