Saturday, April 29, 2017

BABU ALIYEMPATIA UJAUZITO MJUKUU WAKE ATOKOMEA KUSIKOJULIKANA

Na Yeremias Ngerangera,     
Namtumbo.

PAMOJA na Serikali kuendelea kusisitiza wahalifu wanaowapatia mimba wanafunzi wa kike kufungwa miaka thelathini jela, bado baadhi ya jamii imekuwa ikiendelea na tabia hiyo kitendo ambacho kimekuwa kikikatisha ndoto za maendeleo ya maisha kwa watoto hao.

Aidha wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, tabia hiyo imekuwa ikiendelea kufanyika licha ya viongozi husika wilayani humo kukemea kwa nguvu na kupiga marufuku baada ya kuona kwamba imekuwa ikitishia maendeleo ya wanafunzi hao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa tatizo hilo limekuwa likiendelea kushamiri wilayani hapa, kutokana na jamii kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali hasa pale inapotaka kusimamia sheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wenye tabia hiyo.

Imeelezwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha badala yake ndiyo wamekuwa chanzo cha kuvuruga madai husika yasiweze kusonga mbele katika vyombo vya sheria ikiwa ni lengo la kuepuka kufungwa miaka 30 jela.


Hivi karibuni mzee mmoja, Philibert Komba (61) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lukimwa wilayani Namtumbo anadaiwa kumpatia ujauzito mjukuu wake (Jina tunalo) mwenye umri wa miaka 16 ambaye anasoma kidato cha pili shule ya sekondari Lukimwa iliyopo wilayani humo.

Imedaiwa kuwa jamii inayoishi katika kijiji hicho ilikuwa ikifahamu fika tabia ya mzee huyo, baada ya mjukuu wake alipobanwa aeleze ni nani mhusika aliyempatia ujauzito huo ndipo alipomtaja na hatimaye babu huyo alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Shauri hilo lilipofikishwa katika Mahakama ya mwanzo Mkongo wilayani hapa, ndipo binti huyo alibainisha mazingira hayo na kueleza kuwa mzee huyo alikuwa akimfuata chumbani kwake anakolala majira ya usiku na kumlazimisha kufanya naye tendo hilo la ndoa.

“Alikuwa akiingia chumbani kwangu majira ya usiku na kunilazimisha kufanya naye mapenzi, huku akiniambia nikipiga kelele ataniua”, alisema mwanafunzi huyo. 


Hata hivyo Polisi wilayani Namtumbo wamekuwa wakiendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika Mahakama hiyo na kujibu mashtaka hayo yanayomakabili.

No comments: