Wednesday, April 26, 2017

NYASA WAIOMBA SERIKALI KUFANYA DORIA KANDO KANDO YA ZIWA

Na Muhidin Amri,      
Nyasa.

BAADHI ya wananchi wanaoishi katika vijiji vya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi wilayani humo kufanya doria ya mara kwa mara kando kando mwa ziwa Nyasa, ili kuweza kuwachukulia hatua   watu wenye mazoea ya kuoga ziwani wakiwa uchi wa mnyama.

Walisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikichochea na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya ngono zembe, miongoni mwa baadhi ya wananchi wanaoishi wilayani humo na kusababisha maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Kelvin Komba (42) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nkiri wilayani hapa alisema kwamba katika wilaya hiyo hususani vijijini kwenye makambi ya wavuvi, wanaume na wanawake wamekuwa na tabia hiyo tena huoga bila nguo huku wakiwa jinsia tofauti.


Komba alieleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha watu hao hasa wanaume ambao hukaa kwenye makambi hayo kwa muda mrefu bila kukutana na wenzi wao, hushikwa na tamaa ya ngono na kujikuta wakifanya tendo hilo bila kuchukua tahadhari ya kutumia kinga.

Naye Rehema Nchimbi kutoka katika mji wa Mbamba bay wilayani Nyasa alisema hata katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi yaani wanawake na wanaume kumekuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikai katika kukabiliana na maambuzi hayo yakiwemo magonjwa mengine ya zinaa.

Alisema kuwa katika maeneo hayo ya wavuvi hata baadhi ya vijiji vingine watu hupendelea kuchanganyika na watoto wadogo bila kujali umri, hivyo umefika wakati sasa hata kwa viongozi wa serikali za vijiji kuchukua hatua kwa kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kwani inakiuka maadili ya kitanzania.


Pamoja na mambo mengine wameiomba serikali kuchukua hatua madhubuti ya kukomesha tabia hiyo na kupeleka elimu juu ya madhara ya kufanya hivyo ikiwemo gonjwa la ukimwi, hasa katika kambi za wavuvi hao ambako ndiko kumeshamiri vitendo hivyo ili kuweza kunusuru maisha ya watu wengi hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa hili.

No comments: