Friday, April 14, 2017

UGONJWA UNAOUA NGURUWE WAINGIA MBINGA NA KUSHAMBULIA NGURUWE KATIKA KIJIJI CHA KITURA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

UMETOKEA ugonjwa wa nguruwe aina ya African Swain Fever, katika kijiji cha Kitura kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma na kusababisha nguruwe 18 kufa katika kijiji hicho, baada ya kuripotiwa wakiwa na ugonjwa huo.

Aidha imeelezwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo kutokea kijijini hapo umesababishwa na mama mmoja ambaye hakutajwa jina lake akitokea mkoa wa Njombe, baada ya kusafirisha nyama ya nguruwe na kupeleka katika kata hiyo kwa lengo la kubadilishana na zao la kahawa kwa wananchi wanaoishi huko.

Hayo yalisemwa jana na Daktari Mkuu wa mifugo halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Patrick Banzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake huku akieleza kuwa hauna madhara kwa binadamu lakini endapo ukiingia sehemu yoyote ile yenye wanyama hao umekuwa ukiua nguruwe wengi kwa muda mfupi.


“Ugonjwa huu ukiingia kwenye zizi kama kulikuwa na hata nguruwe 100 wote wanakufa mara moja, hivyo tumezuia uchinjaji kuendelea katika maeneo yote yaliyoathirika katika kijiji kile”, alisema Dkt. Banzi.

Pia aliongeza kuwa katika kupambana na ugonjwa huo wa African Swain Fever kwenye maeneo ya kata hiyo ya Kitura, tayari dawa zimepulizwa na wanyama wote waliokufa wamefukiwa.

Dkt. Banzi alifafanua kuwa vilevile wamezuia kwa kutoruhusu kuingiza mifugo au kutoa ndani ya wilaya ya Mbinga, ikiwemo nyama na mbolea za samadi zitokanazo na mnyama huyo.

Alisisitiza kuwa kwa wale wote wanaojishughulisha na uchinjaji wanapaswa pia kuwa na vibali maalumu vya uchinjaji, ambavyo vinawatambulisha wapi wanatoka na mifugo na mifugo yao kuchunguzwa kitaalamu ili isiweze kuleta madhara kwa wengine.


Pamoja na mambo mengine nazo serikali za vijiji wilayani humo zimesisitizwa kutenga maeneo maalumu ya uchinjaji na kwamba kwa wale wote watakaokiuka utaratibu huo watatozwa faini ya shilingi 300,000 na isiyozidi 500,000 au kushtakiwa mahakamani na kwenda jela kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja.

No comments: