Friday, June 2, 2017

DOKTA MAHENGE AMTAKA MKURUGENZI MANISPAA SONGEA KUWALIPA FIDIA WANANCHI KATA YA SUBIRA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Songea (Hawapo pichani) katika ziara ya siku moja ya kukagua usafi wa mazingira katika mji wa Songea mkoani humo.
Na Mwandishi wetu,    
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma, imetoa agizo kwa kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani humo, Tina Sekambo kuwalipa fidia shilingi milioni 22 wakazi wa kata ya Subira katika Manispaa hiyo, ambao eneo lao lenye ekari 25 limetwaliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa dampo la kisasa la kuhifadhia taka.

Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Manispaa hiyo katika ziara yake ya siku moja ya kukagua maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo mjini hapa.

Kadhalika Dkt. Mahenge alisema kuwa wakati Manispaa inatekeleza taratibu za ujenzi wa dampo hilo kuna kila sababu pia ya kutafuta eneo lingine maalum kwa muda nje ya mji huo kwa ajili ya kumwaga taka hizo zinazozalishwa hivi sasa.


Vilevile Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Abdul Mshaweji akizungumzia hilo amemuhakikishia Mkuu wa mkoa huyo kutekeleza agizo hilo mapema ambapo alisema Manispaa ina maeneo mawili nje ya mji huo, ambayo yataweza kutumika kwa muda kutupa taka wakati maandalizi mengine ya ujenzi wa dampo hilo la kisasa unafanyika.

Awali akisoma taarifa ya hali ya uzalishaji taka katika mji wa Songea Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo alisema kuwa Manispaa imekuwa ikizalisha taka kiasi cha tani 71.5 kwa siku, huku uwezo wa kuzoa taka hizo kwa siku ukiwa ni kati ya tani 35 hadi 40 hali ambayo inasababisha tani 31.5 kubaki bila kuzolewa.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa tangu mwezi Januari mwaka huu Manispaa imekosa sehemu maalum ya kutupa taka kutokana na wananchi wa Mwengemshindo ambako taka zilikuwa zinatupwa hapo awali, kuzuia magari yasimwage tena taka huko hivyo kufanya zoezi hilo lisimame kwa muda utekelezaji wake.

Kwa upande wake Ofisa usafi na mazingira wa Manispaa ya Songea, Philipo Beno alisema Manispaa hivi sasa wana jumla ya maghuba 33 ya kuhifadhia taka katika mji huo.

“Idara inatarajia hivi karibuni kupokea kijiko yaani mtambo wa kuzolea taka ambao utarahisisha ukusanyaji wa taka hizi na kupunguza muda wa kuzoa kwa urahisi zaidi”, alisema Beno.





No comments: