Sunday, June 25, 2017

KAMPUNI YA MANTRA TANZANIA LIMITED YATOA MSAADA SHULE ZA SEKONDARI NAMTUMBO

Na Kassian Nyandindi,    
Namtumbo.

SHULE ya Sekondari Korido iliyopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imepata msaada wa shilingi milioni 18.7 kutoka Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, ambazo zimetumika kukarabati chumba cha Maktaba na kununua vitabu kwa ajili ya kuweza kuinua na kuongeza kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.

Kampuni hiyo ambayo inafanya kazi ya kutafiti madini aina ya Uranium One katika mto Mkuju wilayani humo, ndiyo ambayo imetoa msaada huo ikiwemo sehemu ya fedha hizo zimetumika pia kununua vitabu 8,000 vya masomo ya aina mbalimbali.

Khadija Palangyo ambaye ni Afisa mahusiano wa Mantra Tanzania Limited, alisema hayo jana wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mjini hapa.

Vilevile alisema kuwa wamekuwa wakifanya shughuli za kimaendeleo wilayani humo katika jamii ikiwemo utoaji wa misaada kama vile ujenzi wa madarasa shuleni, visima vya maji na utengenezaji wa madawati.


Alifafanua kuwa katika wilaya ya Namtumbo wameweza kujenga Maktaba nne kwa shule mbalimbali za sekondari na kwamba mpaka sasa, zote zimekuwa zikifanya kazi kwa wanafunzi wa shule hizo huzitumia kwa kujisomea ili kuongeza kiwango cha taaluma.

Palangyo alitoa wito kwa wanafunzi wanaotumia Maktaba hizo katika wilaya hiyo, kutunza vitabu na vifaa vyote ambavyo wamepewa ili viweze kuwasaidia katika kujisomea na kuongeza maarifa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Naye kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Luckness Amlima ambaye alikuwa akifungua Maktaba hizo alipongeza jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, hasa katika kuangalia namna ya kusaidia watoto hao wanaosoma katika shule hizo za sekondari.

Amlima alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejiwekea mikakati ya kuboresha sekta ya elimu katika ngazi zote, hivyo wananchi na wadau mbalimbali wanapaswa kuendelea kuunga mkono jitihada hizo ili kuweza kufikia malengo husika.

Pamoja na mambo mengine wilaya ya Namtumbo ina jumla ya shule za sekondari 24 ambapo Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza pia kwa kuwataka wanafunzi wa shule hizo wilayani humo, kutunza vitabu na vifaa vilivyomo kwenye Maktaba hizo ambavyo wamepewa msaada na Kampuni hiyo.

No comments: