Tuesday, June 6, 2017

MKUU WA MKOA RUVUMA ACHUKIZWA NA UCHAFUZI WA MAZINGIRA ZIWA NYASA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akishiriki zoezi la kufanya usafi wa mazingira na wanafunzi wa shule ya msingi Mbamba bay wilayani humo juzi, wakati wa zoezi hilo kandokando ya ziwa Nyasa.
Mkazi wa kijiji cha Mbamba bay wilayani Nyasa, Makrina Matembo upande wa kulia akimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge baada ya mkazi huyo kukutwa akifua nguo kandokando ya ziwa Nyasa na kumwaga uchafu (povu la sabuni) ndani ya ziwa hilo jambo ambalo ni hatari kwa uhai wa viumbe hai waishio ndani ya ziwa, ambapo Dkt. Mahenge alikemea hali hiyo na kutoa maelekezo kwamba vitendo hivyo visiendelee kufanyika kwani vimekuwa na madhara makubwa kwa viumbe hao. (Picha na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

VITENDO vinavyofanywa na baadhi ya Wananchi waishio katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma vya kufua nguo zao na kuosha Pikipiki kandokando ya ziwa Nyasa wilayani humo, vimemchukiza Mkuu wa mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge na kufikia hatua ya kupiga marufuku visiendelee kufanyika ikiwa ni hatua nzuri itakayoweza kudhibiti upotevu wa viumbe hai yakiwemo mazalia ya samaki yaliyopo kwenye ziwa hilo.

Mkuu huyo wa mkoa amepiga marufuku juzi wakati alipokuwa wilayani humo akiongoza na kukagua zoezi la kazi ya kufanya usafi wa mazingira eneo la kijiji cha Mbamba bay, huku akiutaka uongozi wa wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kuzuia vitendo hivyo visiweze kuendelea kufanyika.

“Sikatazi watu kutumia maji ya ziwa hili kwa ajili ya shughuli zao za kila siku isipokuwa ninachokataza hapa, watu wasiende hadi ziwani kufanya shughuli za kufua nguo na kuosha vyombo vyao vya moto badala yake tumieni maji haya kwa kuyachota kwenye chombo maalum na kwenda kuosha hizi nguo zenu mbali na ziwa hili”, alisisitiza Dkt. Mahenge.


Alisema kuwa kwenye vyombo vya moto kama vile Pikipiki kumekuwa na mafuta ambayo ni hatari kwa usalama wa viumbe hai vinavyoishi kwenye ziwa hilo huku akiongeza kwa kuwataka waache mara moja tabia hiyo ya kuharibu mazingira ya ziwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Kufuatia hali hiyo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba kuivunja Kamati ya usimamizi wa mazingira (BMU) wilayani humo kutokana na kukaidi na kushindwa kutekeleza maagizo ya serikali yanayowataka kusimamia na kushiriki kikamilifu zoezi hilo la usafi kila mwishoni mwa mwezi.

Alisema kuwa Kamati hiyo haipaswi kuendelea kuwepo ikifanya kazi ndani ya wilaya hiyo, kwani imeshindwa kutekeleza majukumu yake yakiwemo kuwachukulia hatua baadhi ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa viumbe hivyo ndani ya ziwa Nyasa.

Dkt. Mahenge aliagiza pia kwa kuitaka halmashauri ya wilaya hiyo kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufanyia usafi wa mazingira, ikiwemo magari ya kuzolea taka kwani ni aibu kuona wilaya hiyo haina hata gari moja la kubebea taka au kuwa na kifaa cha kufanyia shughuli za usafi.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Chilumba alimweleza Mkuu huyo wa mkoa kwamba wilaya itaendelea kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za usafi wa mazingira katika maeneo yote, hata hivyo changamoto kubwa ni  kwa baadhi ya wananchi kutoshiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

No comments: