Wednesday, June 21, 2017

WAPOTEZA MAISHA BAADA YA GARI NA TELA LAKE KUACHA NJIA NA KUPINDUKA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WATU   watatu wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti likiwemo la wawili kufa papo hapo, baada ya gari lililokuwa na tela lake likiwa limesheheni makaa ya mawe kuacha njia na kupinduka kisha kutumbukia katika mto Nakatete uliopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Gemin Mushy aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Shaban Msangi (39) ambaye alikuwa ni dereva wa gari hilo lililobeba makaa ya mawe, Haji Yusuph (18) alikuwa ni tingo wa gari hilo wote ni wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani na Cosmas Thadei (80) mkazi wa eneo la Sanangula Manispaa ya Songea.

Alifafanua kuwa katika tukio la kwanza inadaiwa kuwa Juni 20 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Utwango kata ya Namabengo wilayani Namtumbo, gari lenye namba za usajili T 767 DKS lililokuwa na tela lake lenye namba za usajili T 324 DKS aina ya HOWO mali ya Kampuni ya Dangote lilikuwa limebeba tani 25 za makaa ya mawe likitokea Songea kwenda Mtwara.


Gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Msangi ambapo lilikuwa kwenye mwendo kasi liliacha njia na kupinduka, kisha kutumbukia kwenye mto huo ambao upo Kilometa 30 kutoka katika Manispaa ya Songea na kusababisha vifo hivyo vya watu wawili.

Alilitaja tukio jingine kuwa Juni 20 mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika eneo la Sanangula kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe, Pikipiki yenye namba za usajili MC 871 ABA aina ya Sanlg iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye jina lake halikuweza kufahamika ilimgonga mtembea kwa miguu, Cosmas Thadei mkazi wa eneo hilo na kusababisha kifo papo hapo na dereva wa Pikipiki hiyo baada ya kubaini amesabisha kifo alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Miili ya marehemu hao watatu hivi sasa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya mkoa wa Ruvuma Songea, ikisubiri ndugu wajitokeze kwenda kuichukua kwa ajili ya mazishi na kwamba Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kumtafuta mwendesha bodaboda huyo ambaye amekimbia na kuitelekeza Pikipiki yake.


Kwa ujumla imefafanuliwa kuwa chanzo cha ajali zote mbili ni mwendo kasi ambao ulisababisha madereva hao kushindwa kudhiti vyombo vyao vya moto wakati walipokuwa wakiendesha.

No comments: