Friday, June 2, 2017

WANANCHI KATIKA MJI WA MBINGA WAPONGEZA ZOEZI LA UZOAJI TAKA


Ofisa afya wa halmashauri ya Mji wa Mbinga, Felix Matembo akisimamia zoezi endelevu la uzoaji taka katika maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo katika mji huo.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WAKAZI wa Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamepongeza hatua ya serikali kwa kuchukua hatua za haraka katika kuusafisha mji huo ambao ulikuwa katika hali mbaya ya uchafu na kuhatarisha usalama wa afya, kwa wakazi wanaoishi mjini hapa.

Aidha walisema kuwa hali ya maghuba ya kuhifadhia taka kwenye mji huo awali ilikuwa mbaya kutokana na taka nyingi kukaa kwa muda mrefu bila kuzolewa na kuzagaa hovyo, hivyo hatua iliyochukuliwa ya kuziondoa ni jambo la busara ambalo sasa linawafanya wananchi waweze kuishi katika mazingira mazuri.

Hayo yalisemwa na wakazi wa mji wa Mbinga kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, juu ya zoezi endelevu ambalo linafanyika mjini hapa katika kuuweka mji huo katika hali ya usafi.

Kwa upande wake alipohojiwa Ofisa afya wa mji huo, Felix Matembo alieleza kuwa awali zoezi hilo walikuwa wanashindwa kulitekeleza ipasavyo kutokana na kukosa rasilimali fedha, magari ya kuzolea taka na vifaa kwa ujumla vya kufanyia kazi hiyo lakini hivi sasa wameanza kutekeleza zoezi la uzoaji wa taka hizo kulingana na vifaa vichache walivyonavyo.


“Tunawashukuru sana wadau mbalimbali hapa Mbinga mjini kwa kujitokeza katika kuchangia vifaa hivi ambavyo leo hii vinatuwezesha kutekeleza zoezi hili kwa ufanisi mzuri, vinginevyo halmashauri peke yake isingeweza kufanya usafi huu kwa mara moja bila uwepo wa vifaa hivi ambavyo vinatusaidia kuzoa taka hizi na kuzibeba katika magari na kwenda kuzitupa kwenye eneo maalum ambalo limetengwa kwa ajili ya kuteketeza taka hizi”, alisema Matembo.

Matembo aliongeza kuwa halmashauri ya mji wa Mbinga katika mipango yake ya maendeleo imejiwekea pia bajeti ya kununua vifaa maalum vya kuzolea taka ndani ya mji huo, hivyo hapo baadaye vitakapopatikana hali ya usafi itaendelea kuimarika na jamii itaweza kuondokana na kero hiyo.

Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa uwezo wa halmashauri hiyo kuzoa taka hizo katika maghuba 18 yaliyopo mjini hapa upo, hivyo wataendelea kutilia mkazo suala hilo na sio kulifanyia uzembe kwa kuacha taka zirundikane kwa muda mrefu kwenye maghuba hayo.


Hata hivyo alisisitiza kuwa mji huo hautakiwi kuwa katika hali ya uchafu lengo la kufanya hivyo ni kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, ambapo uongozi wa mji utaendelea kusimamia masuala ya usafi kwa kushirikisha jamii katika maeneo yao wanayoishi ikiwemo kuchangia kidogo gharama za uzoaji taka na usafi kwa ujumla ndani ya mji. 

No comments: