Saturday, June 24, 2017

DIWANI WA CHAMA CHA MAPINDUZI HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA AFARIKI DUNIA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

DIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mhongozi, Emeran Cyprian Mapunda (54) katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma amefariki dunia katika Hospitali ya Misheni Peramiho iliyopo mkoani humo, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose Nchimbi alimweleza mwandishi wetu kuwa diwani huyo amefikwa na mauti usiku wa Juni 23 mwaka huu wakati alipokuwa katika hospitali hiyo.

Nchimbi alifafanua kuwa kufariki kwa diwani Mapunda kumesababishwa na tukio la kuanguka Juni 22 mwaka huu akiwa amepanda juu ya mti, wakati alipokuwa akisafisha shamba lake la kahawa katika kijiji cha Mhongozi kilichopo kwenye kata hiyo.


“Katika mashamba yetu ya kahawa tumekuwa na tabia ya kupanda miti ya kivuli, hivyo alikuwa akikata matawi katika miti iliyopo kwenye shamba lake la kahawa ndipo alipokuwa akishuka kutoka kwenye mti huo kwa bahati mbaya alianguka akiwa ametanguliza kichwa”, alisema Nchimbi.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Madaktari wa hospitali hiyo wamethibitisha kifo hicho wakisema kuwa, kimetokana na kuanguka kwake ambako kulisababisha mshipa mkuu wa mgongoni kupishana na kupoteza mawasiliano na mishipa ya fahamu iliyopo kichwani.

Alisema kuwa wakati halmashauri hiyo ilipokuwa inafanya utaratibu wa kumsafirisha kwa njia ya ndege kwenda hospitali ya taifa Muhimbili, ndipo majira hayo ya usiku alifariki dunia.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema kuwa chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa kufariki kwa diwani huyo.

“Sisi kama chama limetushitua tukio hili kupoteza kada wetu ndani ya chama, kata na wananchi aliokuwa akiwaongoza lakini yote haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu”, alisema Mbunda.

Pamoja na mambo mengine, marehemu Mapunda ameacha mke na familia ya watoto sita na kwamba mazishi yake yatafanyika Juni 25 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika makaburi ya kijiji cha Mhongozi kata ya Mhongozi wilayani Mbinga.

No comments: