Monday, June 12, 2017

KAMPUNI YA KUCHIMBA MADINI ACACIA ILIINGIA KINYEMELA HAINA KIBALI CHOCHOTE CHA KUFANYA KAZI HAPA NCHINI

Na Mwandishi wetu,

IMEELEZWA kuwa Taarifa ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyopo kwenye Makontena yenye mchanga wa madini iliyoundwa na Rais Dkt. Joseph Magufuli, imebaini kuwa Kampuni ya ACACIA Mining Plc haina kibali na inafanya kazi kinyume cha sheria hapa nchini.

Profesa Osoro alisema hayo kwamba Kamati yake imebaini madudu hayo kuwa Kampuni hiyo haina uhalali wa kufanya shughuli zake Tanzania na imetenda makosa yakiwemo kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, uhujumu uchumi, jinai na kulitia hasara taifa.

Aidha Kamati ya Profesa Osoro imebaini kwamba Makinikia yaliyouzwa nje ya nchi hayakuwa Makinikia hasa, bali yalikuwa ni madini mbalimbali huku ikiongeza kwamba katika mikataba ya uuzwaji wa Makinikia hayo, serikali haikuwa sehemu ya mikataba hiyo.

Vilevile aliongeza kwamba jumla ya mapato yote ambayo serikali imepoteza ni shilingi trilioni 68.6 sawa na bajeti ya miaka miwili ya nchi, kodi ya mapato ambayo taifa imepoteza ni shilingi trilioni 55.07, mrahaba trilioni 11, bandari trilioni 1.6. na kwamba jumla ya thamani ya madini kwenye makontena yote 44,277 tangu mwaka 1998 ni shilingi trilioni 132.56.

Pamoja na hayo kadhalika imebainika kuwa uongezwaji wa leseni kinyume cha sheria ambapo imedaiwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Sospeter Muhongo ndio waliohusika na uongezaji wa muda kwenye uchimbaji wa madini hayo.

Kamati hiyo imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwepo kuchukua sheria juu ya Kampuni ya ACACIA iliyopo nchini kinyume cha sheria kupitia msajili wa makampuni ikiwa ni pamoja na Mawaziri wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine juu ya mikataba ya uchimbaji madini huku ikiitaka Serikali iwe inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye makampuni hayo ya madini.






No comments: