Wednesday, June 21, 2017

SONGEA WAMPONGEZA RAIS DKT. MAGUFULI KATIKA KUDHIBITI WIZI WA RASILIMALI ZA NCHI

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

JITIHADA zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli katika kudhibiti vitendo vya wizi wa rasilimali za nchi yakiwemo madini, zimepongezwa na baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa kata ya Mateka katika Manispaa hiyo, Kazira Hussein.

Rais Dkt. John Magufuli.
Wananchi hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa kitendo cha Rais Dkt. Magufuli kubaini mbinu chafu zilizokuwa zinafanywa na viongozi ambao siyo waaminifu, ambao walikuwa wakiidanganya serikali kwamba wanasafirisha mchanga usiokuwa na madini na kuupeleka nje ya nchi, wakati mchanga huo ulikuwa na madini ni jambo ambalo linasikitisha na kudhihirisha kuwa kwa muda mrefu Watanzania walikuwa wanaibiwa.

Joseph Milanzi mkazi wa Lizaboni alieleza kuwa kazi inayoendelea kufanywa na Rais huyo katika kuwabaini wahalifu hao, inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote ili kuweza kulifanya taifa liweze kukua kiuchumi kupitia rasilimali zake na sio muda mwingi kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.


Kazira Hussein ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Mateka iliyopo mjini hapa alisema kuwa sifa ya Rais Dkt. Magufuli inazidi kukonga mioyo ya Watanzania wengi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa na uchungu kutokana na wizi huo wa madini na mikataba mibovu iliyokuwepo ambayo ilisababisha wizi huo uendelee kufanyika.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wananchi wengi walikuwa wakishindwa kupata huduma za msingi kama vile afya, kilimo na elimu ikiwemo kupunguza makali ya maisha ambayo wamekuwa wakiendelea kupambana nayo hadi sasa.

Kadhalika Herman Komba mkazi wa Msamala naye aliongeza kuwa kiongozi huyo Watanzania hawakukosea kumchagua kwani ameonesha msimamo wa hali ya juu ambao hata wananchi na wanasiasa wengine wamekuwa mstari wa mbele kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kupigania haki ya wananchi wake.


Pamoja na mambo mengine wananchi hao wa Manispaa ya Songea walisema kuwa kuna kila sababu kwa Watanzania kuona umuhimu wa kufanya maandamano ya amani nchi nzima, ambayo yatalenga kumpongeza Rais Dkt. Magufuri na kuzungumzia mstakabali mzima wa uchumi wa nchi yetu huku wakiliomba hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya kazi kwa makini hasa pale wanapojadili na kupitisha mikataba yenye maslahi na taifa hili.

No comments: