Wednesday, June 14, 2017

HALMASHAURI YA NYASA IMEANZA UJENZI WA BARABARA ZAKE KWA KIWANGO CHA CHANGARAWE

Ziwa Nyasa.
Na Muhidin Amri,     
Nyasa.

HALMASHAURI wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, imeanza kazi ya ujenzi wa barabara zake za mitaa kwa kiwango cha changarawe ikiwa ni mpango wa kuboresha barabara hizo, ili ziweze kuwa katika hali nzuri na kurahisisha kukua kwa maendeleo katika wilaya hiyo hususan usafirishaji mazao kutoka shambani hadi sokoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Oscar Mbyuzi alisema hayo juzi wakati wa zoezi la ufunguzi rasmi ujenzi wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa nane katika kijiji cha Kilosa wilayani hapa.

Dkt. Mbyuzi alisema kuwa mradi huo ulianza tangu mwezi Februari mwaka huu na kwamba utakuwa endelevu kila halmashauri yake itakapokuwa na fedha za kutosha kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.


Wilaya ya Nyasa ina jumla ya kilometa 45 za barabara za mitaa ambazo zimeainishwa kisheria na kupimwa katika mpango wa mipango miji ambapo wilaya hiyo, imejiwekea mikakati ya kuboresha barabara zake kutoka kiwango cha udongo hadi changarawe kilometa tano kwa kila mwaka ili ziweze kuwa bora zaidi na kufanya zipitike kwa kipindi chote cha mwaka.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mradi wa barabara kilometa nane za mitaa hadi sasa umegharimu jumla ya shilingi milioni 170,235,897 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu shilingi 161,164,636 na mchango wa halmashauri ni shilingi 9,071,261.

Aidha alisema kuwa licha ya barabara hizo kujengwa kwa kiwango hicho zitasaidia pia kuimarisha maendeleo ya vijiji vitakavyopitiwa na mpango huo kuwa na muonekano mzuri, sambamba na kuvutia watalii watakao kuwa wakienda wilayani humo kwa ajili ya shughuli za utalii.


Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutumia fursa zilizopo ndani ya mkoa huo, kwa ajili ya kuwekeza miradi  mbalimbali ya kiuchumi wilayani Nyasa kama vile ujenzi wa hoteli za kisasa kwani kufanya hivyo kutasaidia uwepo wa ongezeko kubwa la watalii wanaotoka ndani na nje ya nchi.

No comments: