Friday, June 16, 2017

WANAWAKE KIGONSERA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI

Na Muhidin Amri,      
Mbinga.

WANAWAKE zaidi ya 150 kutoka katika vijiji vitatu kata ya Kigonsera Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamepata mafunzo ya ujasirimali na kufanikiwa kujiunga kwenye vikundi vinavyowawezesha kujijenga kiuchumi kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Akizungumza  jana wakati wa kufunga mafunzo hayo Diwani wa viti maalum  wa tarafa  ya Kigonsera wilayani humo, Amina Kapinga  alieleza kuwa mbali na wanawake hao kunufaika na elimu hiyo ya ujasirimali pia baadhi yao wameanza kupewa mikopo ya fedha na pembejeo za kilimo kupitia vikundi hivyo.

Kapinga alifafanua kuwa mikopo na fedha hizo wamepata kutoka kwenye taasisi mbalimbali na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS).

Alisema kuwa katika kata hiyo tayari vikundi vitatu vya Mwongozi na Kitumbalomo ambavyo hujishughulisha na shughuli za kilimo na vingine vinavyotengeneza sabuni na nguo aina ya batiki vimeweza kunufaika na mikopo hiyo.


Lengo kubwa la wanawake hao kuanzisha na kujiunga katika vikundi hivyo ni kuweza kupata mikopo ya kuendeshea shughuli zao hususan katika sekta ya kilimo, kwani mpaka sasa ni asilimia 90 tu ndio ambao hujishughulisha katika sekta hiyo muhimu.

Diwani huyo alibainisha kuwa shughuli hizo wanazozifanya huwawezesha pia kupata fedha kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kiuchumi, kusomesha watoto wao, ujenzi wa nyumba bora na hata kununua vyombo vya usafiri ambavyo huwasaidia kurahisisha majukumu yao ya kazi za kila siku.

Kapinga alisema, mafunzo hayo kwa wanawake hao yalitolewa na wataalamu kutoka taasisi za kifedha (Benki) chini ya udhamini wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama ambayo yalifanyika mjini Songea mkoani humo.

“Nawaomba hata watu wengine binafsi na taasisi nyingine za kifedha zijitokeze kuwasaidia hawa wanawake kuwapatia mikopo ya fedha, ili waweze kuimarisha vikundi vyao kwa sababu ukimsaidia mwanamke umesaidia jamii ya kitanzania kutokana na umuhimu mkubwa wa mwanamke katika familia”, alisema Kapinga.


Alisema kuwa mwanamke anao mchango mkubwa katika familia na taifa kwa ujumla kwani ndiye mzalishaji mkubwa ikilinganishwa na mwanaume, hivyo ni vyema sasa serikali ikaona umuhimu wa kusaidia makundi mbalimbali ya wanawake ambao wamejiunga pamoja kwenye vikundi vya ujasiriamali katika kupambana na umaskini.

No comments: