Thursday, June 22, 2017

KATIBU MKUU UTUMISHI WA UMMA ASISITIZA NIDHAMU KWA VIONGOZI NA WATENDAJI WA SERIKALI HAPA NCHINI

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma.
 Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida, wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro alipowatembelea katika kuadhimisha wiki ya utumishi umma.
Na Mwandishi wetu,
Singida.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi na watumishi wote hapa nchini, kuzingatia nidhamu na maadili ya utumishi wa umma ikiwa ndiyo msingi bora wa utendaji kazi ili utumishi wao uweze kuwa mzuri.

Dkt. Ndumbaro alisema hayo leo alipokutana na watumishi wa mkoa wa Singida na kusikiliza matatizo, kero, changamoto pamoja na kupata maoni ya namna ya kuboresha utumishi wa umma kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma nchini.

Alisema kuwa kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu huku akisisitiza viongozi hasa wa watumishi wa umma, kuwasikiliza watumishi wao pale wanapotoa maoni yao bila kuyapuuza au kuwakatisha tamaa kwa vitisho.


“Ukiwa kiongozi unapaswa uweze kuishi na kila aina ya mtu, kuna watumishi wengine hawawezi kufichaficha mambo ukikosea wanakusema bila kupepesa maneno, wengine ni waoga hawawezi kukueleza wazi ila wanatumia mbinu mbalimbali, ukiwa kiongozi uwe tayari kupokea ushauri ili uweze kuboresha utendaji wako”, alisisitiza Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro aliwaasa viongozi hao kuwapongeza watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu ili iwe motisha kwa wale wavivu, huku akiwataka kuwachukulia hatua wale wazembe ambao hawataki kufuata kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

“Unakuta mtumishi anajituma anafanya kazi kwa bidii ana nidhamu na ni mbunifu lakini wewe kiongozi wake unamuangalia tu bila hata ya kumpongeza hiyo inakatisha tama, inatakiwa umpongeze sio lazima umpe fedha hata barua tu ya kutambua utendaji wake itampa hamasa yeye na wenzake lakini pia kuna mwingine anakuwa hatekelezi wajibu wake unamtazama tu, hapo utawakatisha tamaa hata wale wachapakazi wengine”, alisema.

Aidha aliwapongeza watumishi wenye vyeti halali huku akieleza kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi bado ni endelevu ili kuhakikisha kwamba watumishi wanaobaki serikalini ni wale wanaostahili tu huku akiwashauri watumishi kuhakikisha wanasafisha taarifa zao muhimu ziwe halali na sahihi wakati wote.

Naye Katibu tawala mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi alimshukuru Katibu Mkuu Utumishi wa umma, Dkt. Ndumbaro kwa kuwatembelea watumishi wa mkoa wa Singida na kusikiliza changamoto pamoja na maoni yao huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kwamba wataendelea kuchapa kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu.

Dkt. Lutambi alisema watumishi mkoani Singida wanaadhimisha wiki ya Utumishi wa umma, kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuongeza muda wa kufanya kazi kutoka saa tisa na nusu mchana mpaka saa kumi na nusu jioni ili kutoa muda zaidi wa kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iramba Linno Mwageni, naye alimshukuru Katibu Mkuu huyo Utumishi wa umma kwa kutembelea mkoa wa Singida na kutoa maoni yake ili kuboresha utendaji hasa wa serikali za mitaa na kwamba alieleza kuwa serikali inabidi iwaajiri watendaji wa vijiji na kata wa kutosha ili kuweza kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwenye maeneo hayo.


Mwageni alisema kuwa wanaotekeleza shughuli na miradi ya serikali kwa ngazi ya mwananchi hasa maeneo ya vijijini na kata ambao hivi sasa ni wachache ni hao watendaji hivyo serikali haina budi kuwaajiri wengine ili waweze kutosheleza katika maeneo hayo hasa katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

No comments: