Sunday, June 18, 2017

DIWANI KATA YA KITANDA AOMBA RADHI NA KUKIRI KUFANYA UBADHIRIFU MALI ZA WANANCHI MBELE YA VIONGOZI WA CCM


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

HATIMAYE Diwani wa kata ya Kitanda, Zeno Mbunda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma amejikuta akiendelea kuwa katika wakati mgumu baada ya kusimama mbele ya kikao maalumu na kuwaomba radhi baadhi ya Wananchi na Wajumbe wa Baraza la maendeleo la kata hiyo, huku akikiri kwamba tuhuma anazotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa mali na fedha za wananchi hao kuwa ni za kweli.

Zeno Mbunda, Diwani kata ya Kitanda.
Pamoja na diwani huyo kukubali makosa hayo mbele ya kikao hicho kilichofanyika Juni 17 mwaka huu kwenye Ofisi za makao makuu ya kata ya Kitanda, aidha alieleza kuwa ifikapo Julai Mosi mwaka huu atakuwa amelipa mali na fedha zote ambazo anadaiwa kutofikisha katani humo.

Radhi hiyo ambayo alikuwa akiiomba mbele ya ushuhuda wa viongozi wa CCM wilaya ya Mbinga, akiwemo na Mwenyekiti wa Chama hicho Christantus Mbunda ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho.

Licha ya kuwaomba radhi bado Wajumbe wa baraza hilo la maendeleo la kata walionekana kutoridhishwa na hali hiyo huku wengine wakisema kuwa hawawezi kuchukua hatua ya kumsamehe, kwani ni mapema mno mpaka pale atakaporejesha mali na fedha za wakulima wa kahawa anazotuhumiwa kuzitafuna kwa manufaa yake binafsi.

“Hatuwezi kuchukua hatua ya kumsamehe mpaka pia tupate majibu ya hatua zilizochukuliwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya, ambako malalamiko haya tuliyapeleka kwa njia ya maandishi na bado hatujajibiwa mpaka sasa”, alisema Mwenyekiti wa kata ya Kitanda Philibert Mkolwe.


Mkolwe aliongeza kuwa hawaoni sababu ya kuendelea kuwa na kiongozi ambaye ni mwizi wa mali za wananchi ni vyema achie madaraka kwani mpaka sasa amesababisha kupungua kwa moyo wa kufanya shughuli za maendeleo ndani ya kata.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda akizungumza katika kikao hicho maalumu ambacho kililenga kutafuta suluhisho la mgogoro huo, licha ya kuwasihi Wajumbe wa mkutano huo wamsamehe diwani wao hali ilizidi kuwa mbaya ambapo waliendelea kujenga msimamo wao wakieleza kuwa hawawezi kumsamehe mtu ambaye ananyoshewa kidole kufanya ubadhirifu wa mali za umma.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa anakubaliana na Wajumbe hao kwamba anapaswa kulipa kwanza mali na fedha za wananchi ndipo wamsamehe kwa kupita tena katika kila vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo kwa kufanya mikutano na wananchi hao kuwaomba radhi kwa makosa aliyowafanyia.  

Kufuatia uwepo wa hali hiyo, Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya aliongeza kuwa kuanzia sasa diwani huyo hatakiwi kuonekana tena anashiriki kwenye shughuli za manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi, badala yake anapaswa kumwachia Afisa mtendaji wa kata hiyo ambaye ndiye mhusika mkuu wa kusimamia shughuli hizo na yeye anabakia kuwa ni mfuatiliaji wa shughuli hizo kuona kama zinatekelezwa ipasavyo au la.

Pamoja na mambo mengine, hapo awali kufanyika kwa kikao hicho kunafuatia hatua ya Wajumbe hao kumkataa diwani Mbunda, baada ya kutoa malalamiko yao kwa kuandika barua kwenda Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga, wakimtuhumu kufanya ubadhirifu huo wa mali za wananchi wake.

Barua hiyo ya malalamiko iliyoandikwa Mei 25 mwaka huu ambayo nakala yake tunayo ikiwa na majina na sahihi za mahudhurio ya Wajumbe hao, wameiomba serikali ichukue hatua dhidi ya kiongozi huyo kwa lengo la kuweza kunusuru maendeleo ya wananchi wa kata hiyo.

Sehemu ya barua hiyo inasema kuwa kutokana na kikao cha baraza hilo la kata ya Kitanda kilichofanyika kwa pamoja, walikubaliana kutomuamini tena diwani wao na kumkataa kwa sababu ya kupokea mipira (Roll) kumi ya maji kutoka kwenye mfuko wa Jimbo la Mbinga mjini na kutowasilisha kwa wananchi wa kitongoji cha Matengo kijiji cha Masimeli kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.

Pia wanamtuhumu kufanya upotevu wa vifaa vya ujenzi ambavyo ni saruji, nondo na bati za kuezekea baadhi ya majengo katika shule ya Sekondari Ngwilizi iliyopo katika kata hiyo, vifaa ambavyo vilitolewa na mfuko huo wa jimbo kupitia usimamizi wake na kusababisha vifaa hivyo kupelekwa shuleni hapo vikiwa pungufu huku wakidai pia alipokea msaada wa fedha taslimu shilingi milioni 2 toka kwa Shirika la Masista wa Chipole lililopo wilayani hapa na kutozifikisha kwa Kamati ya ujenzi ya shule hiyo ya Sekondari ili ziweze kusaidia katika kazi ya ujenzi.


Vilevile wanadai kuwa diwani huyo wa CCM ameshiriki kukusanya kahawa ya wakulima kupitia kikundi cha Mjimwema kilichopo kwenye kijiji cha Masimeli, msimu wa mavuno ya zao hilo mwaka 2016/2017 na kutowapa malipo yao wakulima hao baada ya kuiuza kahawa yao ambayo ni zaidi ya tani kumi.

No comments: