Saturday, June 24, 2017

DEREVA APOTEZA MAISHA ABIRIA WAJERUHIWA VIBAYA BAADA YA BASI KUGONGANA USO KWA USO NA LORI LILOBEBA MAKAA YA MAWE

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

DEREVA wa Kampuni ya Super Feo, Ismail Shaban Nyami (38) mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, amefariki dunia papo hapo baada ya basi alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na lori ambalo limebeba makaa ya mawe na kusababisha abiria kumi na moja kujeruhiwa vibaya.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gemin Mushi alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa huku akieleza kuwa tukio hilo lilitokea Juni 22 mwaka huu majira ya jioni katika eneo la Msalaba, lililopo katika kijiji cha Mbangamawe barabara ya kutoka Songea kwenda Njombe na kwamba abiria hao wamelazwa katika hospitali ya mkoa Songea.

Alilitaja gari ambalo lilikuwa limebeba abiria hao kuwa ni lenye namba za usajili T 213 BNU aina ya Yutong ambapo liligongana na gari lenye namba za usajili T 159 CEX aina ya Iveco Stralis likiwa lenye tela namba za usajili T 206 CHS mali ya Kampuni ya Trank Link Limited ya Jijini Dar es Salaam.


Kadhalika alifafanua kuwa basi la Super Feo lilikuwa limebeba abiria 46 likitokea Mbeya kwenda Songea, huku gari hilo lililobeba makaa ya mawe lilikuwa likitokea kwenye mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo.

Chanzo cha ajali hiyo ni kwamba Lori hilo lenye makaa ya mawe lilikuwa kwenye mwendo kasi na kwamba lilikosa mwelekeo na hatimaye kuligonga basi hilo na kusababisha dereva wa basi kupoteza maisha na abiria kujeruhiwa.

Kamanda Mushi aliwataja majeruhi hao kuwa ni Salome Challe (25) mkazi wa Bombambili, Winfrida Chitanda (31) mkazi wa Mbeya, Fransisca Nyari (22) mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Irene Malisa (15) mkazi wa Mbeya, Oresto Nyoni (58) mkazi wa Matarawe Manispaa ya Songea, Noela Ndunguru (25) mkazi wa kijiji cha Kihungu wilayani Mbinga, Anifrida Lameck (30) mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Mariam Salehe (30) mkazi wa Mbeya mjini, Ebron Geitani (4) mkazi wa Vwawa wilayani Mbozi mkoa wa Songwe, Paulina Mnimbo (25) na Joseph Elia (47) wote wakazi wa Songea mjini.


Hata hivyo aliongeza kuwa majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu hospitali ya mkoa wa Ruvuma Songea na kwamba kati yao sita wana hali mbaya ambapo Jeshi la Polisi mkoani hapa, linamtafuta dereva wa Lori hilo ambaye amekimbia hajulikani alikoelekea baada ya ajali hiyo kutokea.

No comments: