Wednesday, June 7, 2017

WAANDISHI WA HABARI WATANGAZAJI WAPIGWA MSASA DODOMA

Washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea na mafunzo katika ukumbi wa Dear Mama uliopo mjini Dodoma.

Mkufunzi wa mafunzo hayo Dotto Bulendu akiendelea kuelimisha Wanahabari (Hawapo pichani) juu ya misingi bora ya uandishi wa habari za utangazaji wa Redio na Televisheni. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Kassian Nyandindi na Magesa Magesa,      
Dodoma.

IMEELEZWA kuwa mafunzo ya utangazaji ambayo yanaendeshwa kwa Waandishi wa habari mkoani Dodoma, yataweza kuwasaidia wanahabari hao katika kufanya kazi zao kwa weledi na misingi bora ambayo itawafanya waendane na zama hizi za Sayansi na tekinolojia.

Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Kamati ya maadili kutoka Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Salma Abdul wakati alipokuwa akifungua mafunzo hayo ya siku nne, ambayo yamefadhiliwa na umoja huo yanayofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Dear Mama iliyopo mjini hapa.

“Sisi ni watu ambao tutakuwa bora zaidi kutokana na utangazaji wetu kuwa mzuri ukizingatia kwamba hivi sasa mtangazaji ndio kila kitu, hivyo tunapaswa wakati wote kuzingatia maadili ya kazi zetu”. alisema Salma.


Vilevile kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dotto Bulendu kutoka Chuo kikuu cha SAUT mkoani Mwanza alisema kuwa kutokana na watu wa redio kuwa na ushindani mkubwa na watu wa televisheni, waandishi wa habari wanapaswa kuendana na wakati kwa kuwa wabunifu zaidi katika kuandika habari zao.

Bulendu alisema kuwa ubunifu huo endapo watazingatia katika ufanyaji wa kazi zao za kila siku utasaidia kuwafanya wasikilizaji kupenda zaidi kusikiliza habari zao kwa kuwa zitakuwa zimezingatia maadili na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Unapoandika habari yako ni lazima uzingatie wasikilizaji wako wanahitaji nini na ili iweze kuwa na matokeo mazuri lazima uzingatie haya tunayojifunza sasa, bila kusahau ubunifu mzuri wa maneno ambayo yatafikisha ujumbe mzuri kwa jamii”, alisisitiza Bulendu.

Hata hivyo washiriki waliopo katika mafunzo hayo ni wa kutoka katika Klabu za waandishi wa habari mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, Simiyu, Singida, Arusha, Geita, Kagera, Mtwara, Mara, Tabora na Lindi.






No comments: