Friday, June 2, 2017

MASHINDANO YA UMISSETA YAFUNGULIWA RASMI MKOANI RUVUMA WASHIRIKI WAONYWA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

MASHINDANO Umoja wa Michezo na Sanaa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) kwa mwaka huu, yamefunguliwa rasmi katika mkoa wa Ruvuma kwenye viwanja vya michezo katika chuo cha ualimu Songea mkoani humo.

Ufunguzi huo ulifanywa juzi na Ofisa elimu wa mkoa huo, Gharama Kinderu kwa niaba ya Katibu tawala mkoa ambapo aliwapongeza washiriki wote waliotoka katika wilaya tano za mkoa huo kwa jitihada zao walizofanya katika kushiriki kikamilifu mashindano hayo.

Kinderu aliwaasa walimu na wanamichezo wote kwa ujumla kuwa na nidhamu na utii wakati wanapokuwa katika mashindano hayo na kwamba ufunguzi wa mashindano hayo utawezesha kupatikana timu ya mkoa wa Ruvuma baada ya mchujo wa vijana kufanyika toka katika kila wilaya.

“Michezo inahitaji nidhamu na jitihada ili uweze kushinda ni jukumu la walimu kuhakikisha mnasimamia nidhamu ya wanafunzi hawa ili waweze kupata ushindi na kuleta sifa nzuri katika mkoa wetu”, alisema Kinderu.


Awali akitoa taarifa ya UMISSETA Mratibu wa mashindano hayo, Yovin Mapunda alieleza kuwa jumla ya wanamichezo 420 na walimu 56 toka wilaya tano za mkoa huo, wamekutana kwa lengo la kuunda timu ya mkoa itakayokwenda kushiriki mashindano ya taifa mkoani Mwanza mwezi Juni mwaka huu.

Aliongeza kuwa kati ya wanamichezo hao wavulana ni 265 na wasichana 196 ambao watashindana katika michezo tisa ili kupata timu ya mkoa kuanzia Mei 28 hadi 30  mwaka huu.

Mapunda aliitaja michezo inayoshindaniwa kuwa ni soka wavulana, soka wasichana, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa wavu, riadha wavulana, riadha wasichana, mpira wa kikapu, mpira wa meza na bao.

Kwa mujibu wa ratiba timu ya mkoa itakayoundwa itakaa kambini kuanzia Mei 31 hadi Juni 03 mwaka huu na kwamba itaelekea Mwanza kwa ajili ya kufanya mashindano ya UMISSETA Taifa.

Kinderu alionya pia dhidi ya vitendo vibaya vya upendeleo vinavyoweza kufanywa na walimu akitaka viachwe mara moja visifanyike, ili vijana hao waweze kwenda kushiriki michezo hiyo wakiwa na sifa nzuri ambapo atakayebainika kujihusisha na njama zozote za kuzorotesha timu ya mkoa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.


Pamoja na mambo mengine Washiriki hao wote wa mashindano hayo wanatoka katika wilaya tano za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.

No comments: